Na John Bukuku
Mkutano Maalum wa Marais na Wakuu wa Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) umefanyika kwa njia ya mtandao tarehe 7 Novemba 2025, ukihusisha viongozi wakuu wa nchi wanachama kujadili masuala muhimu yanayohusu ushirikiano, uongozi na amani katika ukanda huo.
Mkutano huo uliongozwa na Mheshimiwa Matamela Cyril Ramaphosa, Rais wa Jamhuri ya Afrika Kusini, na kuhudhuriwa na Marais na Wakuu wa Serikali, pamoja na wawakilishi wa nchi wanachama wa SADC, wakiwemo Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Emmanuel John Nchimbi; Rais wa Malawi, Prof. Arthur Peter Mutharika; na Rais wa Zimbabwe, Dkt. Emmerson Dambudzo Mnangagwa.
Katika kikao hicho, viongozi wa SADC walituma salamu za rambirambi kwa familia zilizopoteza wapendwa wao kutokana na vurugu na maandamano yaliyotokea nchini Madagascar mwezi Septemba na hivi karibuni nchini Tanzania, wakieleza masikitiko makubwa juu ya vifo na uharibifu wa mali za umma na miundombinu muhimu katika mataifa hayo.
Aidha, Mkutano huo uliwapongeza viongozi waliochaguliwa hivi karibuni akiwemo Rais wa Malawi Prof. Arthur Peter Mutharika, Rais wa Seychelles Dkt. Patrick Herminie, na Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa ushindi wao katika chaguzi za Septemba na Oktoba 2025.
Katika hatua nyingine, viongozi walitambua uamuzi wa Jamhuri ya Madagascar wa kuachia nafasi ya Mwenyekiti wa SADC kufuatia changamoto za kisiasa zilizojitokeza nchini humo. Kwa mujibu wa Ibara ya 9A(2)(b) na 10(4) ya Mkataba wa SADC, Afrika Kusini iliteuliwa rasmi kuwa Mwenyekiti wa Muda wa SADC hadi Agosti 2026, wakati sekretarieti ikiendelea na mchakato wa kumpata Mwenyekiti Mtarajiwa mpya kufikia Novemba 30, 2025.
Mkutano huo pia uliamua kuendelea kutekeleza kaulimbiu ya mwaka 2025/2026 iliyopitishwa mjini Antananarivo, Madagascar, yenye ujumbe: “Kuendeleza Uboreshaji wa Viwanda, Mabadiliko ya Kilimo na Mageuzi ya Nishati kwa Ajili ya SADC Imara.”
Akizungumza baada ya kikao, Rais Ramaphosa alitoa shukrani kwa viongozi wote wa SADC kwa ushirikiano wao na kwa kumchagua kuongoza jumuiya hiyo ya kikanda katika kipindi cha mpito, huku akisisitiza umuhimu wa kudumisha umoja, amani na maendeleo endelevu katika ukanda wa Kusini mwa Afrika.
Kwa upande wake, Rais wa Zimbabwe Dkt. Emmerson Mnangagwa alitoa ofa ya kuandaa baadhi ya mikutano ya SADC nchini mwake katika kipindi cha uongozi wa mpito, kama ishara ya kuendeleza mshikamano na kazi zilizokuwa zimeanzishwa na uongozi uliopita.
Mkutano huo wa SADC ulimalizika kwa wito wa kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi, ulinzi na siasa miongoni mwa nchi wanachama, huku viongozi wakiahidi kuendelea kushirikiana kwa karibu kuhakikisha maendeleo na ustawi wa wananchi wa eneo hilo.



