
Na Mwandishi Wetu, Tunduru
VIONGOZI wa vyama vya msingi vya Ushirika(Amcos) na wakulima wa zao la korosho Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma,wamempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutekeleza mpango wa utoaji wa pembejeo za ruzuku katika msimu wa kilimo 2025/2026.
Wamesema, hatua hiyo itawapunguzia mzigo wa gharama kubwa za uzalishaji na kuongeza tija katika kilimo cha korosho na kuchochea ari ya kufanya kilimo chenye tija.
Wamesema hayo jana kwenye Mkutano wa wadau wa Tasinia ya zao la korosho Mkoa wa Ruvuma uliofanyika katika Ukumbi wa Pili Wilayani Tunduru.
Wamesema, mpango wa pembejeo za ruzuku ulioanza kutekelezwa na Serikali ya awamu ya sita,umeleta mapinduzi makubwa katika kilimo cha korosho kwani umepunguza gharama za uzalishaji kwa wakulima na kuongeza mavuno mashambani.
Rashid Bakari mkulima wa Kijiji cha Nakapanya amesema, kabla ya kutekelezwa kwa mpango huo walikuwa wanatumia fedha nyingi kununua pembejeo hasa Salfa na Viuatilifu kwa ajili ya kupulizia mikorosho hali iliyokuwa ikipunguza faida katika kilimo cha zao hilo.
Bakari amesema, sasa anavuna kati ya gunia 30 hadi 45 kwa ekari moja tofauti na kipindi cha nyuma ambapo mavuno yalikuwa duni kutokana na kushindwa kumudu gharama za maandalizi kwani pembejeo ziliuzwa kwa bei kubwa.
Aidha,amekishukuru Chama kikuu cha Ushirika(TAMCU),kwa kumaliza changamoto mbalimbali ikiwemo upatikanaji wa magunia na viuatilifu ambavyo vilirudisha nyuma jitihada wanazofanya katika uzalishaji wa zao la korosho.
Amesema, katika misimu iliyopita changamoto ya maguni ilikuwa kubwa hivyo kusababisha baadhi yao kushindwa kukusanya korosho kwa wakati hivyo kukosa bei kwenye minada ya kwanza ambayo ina faida kubwa kwa mkulima kwa kuwa makampuni yananunua korosho kwa bei ya juu.
Mkulima mwingine Rashid Mfaume,amemshukuru Rais Samia kuwapa wakulima pembejeo bure ambazo zimechangia kuongezeka kwa uzalishaji wa zao hilo kwenye mashamba yao.
Mfaume,amewapongeza maafisa Ushirika kwa kuhamasisha wakulima waweze kujiunga na ushirika ili kuuza mazao yao kwa mfumo wa stakabadhi ghalani ambao umeleta manufaa makubwa kwao.
Abdala Kawawa kutoka Chama cha Msingi Mnachanga Amcos amesema,sasa wanatamba kwani wanapata pembejeo za ruzuku kwa urahisi ambazo zimehamasisha wananchi wengi wakiwemo vijana kulima korosho.
Hata hivyo,ameiomba Serikali iendelee na mpango wa kutoa pembejeo za ruzuku ili kuhamasisha wananchi hasa vijana wengi zaidi kwenda kuanzisha mashamba ya korosho badala ya kutumia muda mwingi kwenye kilimo cha mzao mengine ambayo yana tija kubwa.
Kawawa,ameshauri Taasisi ya utafiti wa Kilimo Tanzania(TARI)Tawi la Naliendele Mkoani Mtwara,kuwa na programu endelevu za utoaji elimu kwa vitendo kupitia mashamba darasa ili kuwajengea wakulima uelewa wa matumizi ya mbegu bora.
Meneja wa Chama Kikuu cha Ushirika Wilaya ya Tunduru Tamcu Marcelino Mrope,amewahakikishia wakulima kuwa tayari wamesambaza pembejeo kwenye vyama vyote vya msingi vya ushirika na kuwasisitiza kutumia pembejeo kwa malengo ili kuleta tija katika kilimo cha korosho.
Mrope, amewataka wakulima wa korosho na mazao mengine yanayouzwa kwa mfumo wa Ushirika(Stakabadhi ghalani) kuendelea kujisajili na kuhuisha taarifa zao kwenye mfumo wa kidigitali wa pembejeo za ruzuku ili kunufaika na mpango huo.
Naye Meneja wa Bodi ya Korosho Tanzania Tawi la Tunduru Shauri Mokiwa amesema,Mkoa wa Ruvuma na mikoa mingine inayouza korosho kupitia Tamcu katika msimu 2025/2026 inakusudia kukusanya na kuuza korosho kilo 35,000,000.
Amesema,makadirio hayo ni makubwa ukilinganisha na misimu iliyopita kutokana na maandalizi yaliyofanyika na juhudi kubwa za Rais Samia Suluhu Hassan kuwapatia wakulima Viuatilifu na mabomba ya kupulizia mikorosho yanayouzwa kwa bei ya ruzuku.



