Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amelaani vikali matukio ya vurugu na uvunjifu wa amani yaliyotokea Oktoba 29 katika baadhi ya maeneo nchini, akisisitiza kuwa vitendo hivyo havina nafasi katika jamii ya Kitanzania inayojivunia utulivu, heshima na mshikamano.
Akizungumza mara baada ya kuapishwa kwa muhula wake wa pili katika viwanja vya Gwaride vya Jeshi Chamwino Ikulu jijini Dodoma, Rais Samia alisema kuwa matukio hayo yameleta huzuni na hasira kwa Watanzania wote wanaoipenda nchi yao. Alieleza kuwa “Kama taifa, tumesikitishwa sana na matukio ya uvunjifu wa amani, upotevu wa maisha na uharibifu wa mali za umma na watu binafsi.
Kilichotokea siyo Utanzania wetu. Ni jambo lisilokubalika hata kidogo,” alisema Dkt. Samia kwa sauti ya upole lakini yenye uzito mkubwa.
Rais alifafanua kuwa uchunguzi wa awali umebainisha kwamba baadhi ya vijana waliokamatwa wakihusishwa na vurugu hizo wanatoka nchi jirani, jambo linaloonyesha kulikuwa na njama za kimakusudi za kuhujumu amani ya Tanzania.
Alisisitiza kuwa vyombo vya ulinzi na usalama vinaendelea kuchunguza kwa kina ili kuwabaini wote waliohusika na kuhakikisha sheria inachukua mkondo wake.
“Haikushangaza kuona baadhi ya waliokamatwa wakitoka nje ya Tanzania. Vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vinaendelea na uchunguzi wa kina kuhakikisha nchi inarejea katika hali ya kawaida mara moja,” alisema Rais Samia.
Aidha, Rais aliagiza Kamati za Ulinzi na Usalama za Mikoa na Wilaya kuhakikisha wananchi wanaendelea na shughuli zao kwa utulivu, huku akitoa onyo kali kwa wote wanaochochea machafuko, akisema serikali haitasita kuchukua hatua kali kwa mujibu wa sheria.
“Vurugu huishia kupimana nguvu, lakini mazungumzo huleta mshikamano. Tuchague lenye manufaa kwetu kama taifa, kwani usalama wa nchi hulindwa na kila mmoja wetu kwa gharama zozote,” aliongeza.
Dkt. Samia pia aliwataka Watanzania kuendelea kudumisha umoja, upendo na uvumilivu, akisisitiza kuwa Tanzania ni nchi ya amani na itaendelea kubaki hivyo. Alikemea vikali siasa za uchochezi na ubaguzi, akisema kuwa baada ya uchaguzi, taifa lazima liungane na kufanya kazi kwa pamoja kujenga uchumi na maendeleo ya watu.
Watanzania wengi wameunga mkono kauli hiyo, wakieleza kuwa vurugu za Oktoba 29 zimeacha funzo muhimu juu ya thamani ya amani na wajibu wa kila mmoja kulinda hadhi ya taifa.




