Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Hamza S. Johari ametimiza haki yake ya Kikatiba ya kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani katika Kituo Cha Kilimani, Jijini Dodoma tarehe 29 Oktoba, 2025.
Akizungumza mara baada ya kukamilisha zoezi la kupiga kura Mwanasheria Mkuu wa Serikali amewataka Wananchi kuendelea kujitokeza kutimiza haki yao ya Kikatiba kwa kupiga kura kwani hali ya usalama ni shwari.
“Niwaombe Wananchi ambao bado hawajajitokeza wajitokeze watimize haki yao ya Kikatiba kwa kuchagua viongozi wetu kwani hali ni shwari kabisa na zoezi linaendelea vizuri.”
Aidha, Mhe. Johari ameipongeza Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi kwa kuweka utaratibu mzuri unaorahisisha zoezi hilo, ambapo ndani ya muda mfupi mpiga kura anakuwa ametimiza hakli yake ya kupiga kura.
“Niwapongeze Tume kwa kuweka utaratibu mzuri wa kupiga kura ukifika hapa una hakiki jina lako na unaelekea eneo la kupiga kura ndani ya muda mfupi sana unakuwa umemaliza”.
Katika hatua nyingine, Mwanasheria Mkuu wa Serikali ametoa wito kwa Wananchi kuendelea kujitokeza na kushiriki katika zoezi hilo la kupiga kura kwa ajili ya kupata viongozi mbalimbali nchini.
“Niwaombe wananchi wananchi waendelee kushiriki zoezi hili, wagombea wote tulipata nafasi ya kuwasikiliza na leo ndiyo siku yenyewe ya kutimiza haki yetu na kupiga kura”.
Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani unafanyika leo tarehe 29 Oktoba, 2025 kwa Watanzania katika maeneo mbalimbali nchini kuchagua Viongozi wao.


