Na Ashrack Miraji Fullshangwe Media
Benki ya NMB Tawi la Same imeungana na wadau wa elimu kuwatia moyo wanafunzi wa kidato cha nne na kidato cha pili wanaotarajia kuanza mitihani yao mwanzoni mwa mwezi Novemba, huku ikisisitiza umuhimu wa bidii, nidhamu na malengo thabiti katika masomo ili kufikia mafanikio.
Akizungumza katika shule ya sekondari Kibacha, Jana October 28 Meneja wa Benki ya NMB Tawi la Same, Bw. Saad Masawila, alisema benki hiyo itaendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali za umma na binafsi katika kuinua sekta ya elimu, hususan kwa kutoa elimu ya fedha kwa vijana ili kuwaandaa kukidhi mahitaji ya soko la ushindani.
“Soko la ushindani wa kielimu limekuwa kubwa sana. Tunahitaji kuona matokeo mazuri kwa wanafunzi wetu wengi wapate ‘division one’, na hata wakifanya vibaya basi wasishuke chini ya ‘division three’,” alisema Bw. Masawila.
Katika hatua ya kuhamasisha zaidi ari ya kujifunza, benki hiyo iliwakabidhi wanafunzi vitendea kazi mbalimbali vya masomo kama zawadi na motisha ya kuwapa hamasa ya kufanya vizuri kwenye mitihani yao.
Kwa upande wake, Afisa Elimu Sekondari wa Wilaya ya Same, Bi. Neema Lemunge, aliwataka wanafunzi hao kuzingatia mafunzo waliyopatiwa darasani na kutumia muda uliosalia kufanya maandalizi ya mwisho kwa umakini ili kufanikisha ndoto zao.
Nao viongozi wa dini waliohudhuria tukio hilo waliwahimiza wanafunzi kudumisha maadili mema, kuheshimu wazazi na walimu, na kumtanguliza Mungu katika kila hatua ya maisha yao, hususan kipindi cha mitihani na mapumziko.
Mmoja wa wanafunzi wa shule hiyo alitoa shukrani kwa niaba ya wenzake, akisema benki ya NMB imekuwa kama mzazi kwao kutokana na mchango wake mkubwa katika elimu kupitia utoaji wa madawati, vifaa vya kujifunzia, elimu ya fedha na sasa vitendea kazi vinavyowahamasisha kuongeza juhudi katika masomo.
Benki ya NMB Tawi la Same imeendelea kutembelea shule mbalimbali za sekondari wilayani humo, ikiendesha programu za elimu ya fedha na kuwahamasisha wanafunzi kuwa na nidhamu ya kifedha, bidii katika masomo na mtazamo chanya wa mafanikio ya baadaye.






