Na Silivia Amandius, Bukoba
Mji wa Bukoba umefurika shamrashamra za wananchi waliokuwa wakihitimisha kampeni za Chama Cha Mapinduzi (CCM), huku sauti za hamasa na nyimbo za kizalendo zikisikika katika viunga vya mji. Maelfu ya wananchi walijitokeza kumpokea mgombea ubunge wa CCM Jimbo la Bukoba Mjini, Mhandisi Johanseni Mtasingwa, aliyefunga kampeni zake kwa ahadi za maendeleo endelevu.
Akihutubia wananchi, Mhandisi Mtasingwa alisema ataendelea kushirikiana na serikali kukamilisha miradi iliyoanzishwa ikiwemo stendi kuu ya mabasi, soko la Bukoba na ukarabati wa kingo za Mto Kanoni. Pia aliahidi kuimarisha miundombinu ya barabara na kuupendezesha mji wa Bukoba kwa kutekeleza ilani ya CCM kwa vitendo.
“Bukoba itakuwa kitovu cha maendeleo Kaskazini Magharibi mwa Tanzania,” alisema Mtasingwa huku akishangiliwa na mamia ya vijana waliokuwa wamevaa mavazi ya kijani na njano. Alisisitiza kuwa uwajibikaji, ushirikiano na uwazi vitakuwa dira yake katika kuwatumikia wananchi.
Viongozi mbalimbali wa CCM ngazi ya mkoa na taifa walihudhuria tukio hilo na kuwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kesho kupiga kura, wakisisitiza kuwa CCM ndiyo chama chenye dira ya kuendeleza mafanikio yaliyopatikana katika sekta za elimu, afya na miundombinu.




