Na Mwandishi wetu, Mirerani
MWENYEKITI wa chama cha wachimbaji madini Mkoa wa Manyara (MAREMA) Elisha Nelson Mnyawi amesema leo jumatano Oktoba 29 mwaka 2025 wachimbaji madini wa mkoa huo hawatachimba madini kwani watakuwa na kazi moja pekee ya kupiga kura.
Elisha Mnyawi ameeleza hayo baada ya kukaribishwa kuzungumza kwenye mkutano wa kufunga kampeni kwa mgombea ubunge kupitia CCM Jimbo la Simanjiro James Kinyasi Ole Millya na madiwani wanne wa Tarafa ya Moipo.
Ameeleza kwamba wachimbaji madini wa Manyara kesho hawatafanya kazi ya kuchimba madini kwani ni siku ya kupiga kura kwa mgombea urais kupitia CCM Dkt Samia Suluhu Hassan, mgombea ubunge Ole Millya na madiwani wa CCM.
Amesema wachimbaji madini wa Mkoa wa Manyara wanatambua mambo mengi mazuri yalivyofanyika kupitia Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan hivyo watalipa wema wao kwa kura zote za ndiyo kwa CCM.
“Wachimbaji wa Manyara tutamlipa deni letu Mama yetu mchapa kazi, mbeba maono Dkt Samia Suluhu Hassan, mbunge Ole Millya na madiwani wanaogombea kupitia CCM,” amesema Elisha Mnyawi.
Mgombea ubunge wa Jimbo la Simanjiro, Ole Millya ambaye alishawahi kuwa mbunge wa Simanjiro mwaka 2015/2020 ameshukuru Mwenyekiti wa MAREMA kwa kujumuika nao.
“Kaka yangu Elisha Mnyawi tulifanya kazi pamoja kipindi cha nyuma, mnafahamu msimamo wangu wa kusimamia ukweli na kuwatetea wachimbaji,” amesema Ole Millya.



