Na Mwamvua Mwinyi, Kibaha
Oktoba 27, 2025
Mgombea udiwani kupitia CCM kata ya Pangani,Mjini Kibaha John Katele, amefunga kampeni huku akiwataka wananchi wa kata hiyo kujitokeza kwa wingi Oktoba 29, 2025 kushiriki katika uchaguzi mkuu kwa amani na kuichagua Chama Cha Mapinduzi (CCM) ili kuendeleza maendeleo yaliyopo.
Akizungumza katika mkutano wa kufunga kampeni mtaa wa Lumumba, Katele alisema wakati umefika wa kufanya maamuzi sahihi kwa mustakabali wa taifa, kwa kumchagua Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, pamoja na wagombea wote wa CCM .
“Tumeona kazi kubwa iliyofanywa na serikali ya CCM chini ya uongozi wa Dkt. Samia, miundombinu imeboreshwa, huduma za kijamii zimeimarika, na uchumi wetu unazidi kukua” Tarehe 29 Oktoba, twendeni tukapige kura kwa amani, tuchague maendeleo,” alisema Katele.
Aliwahimiza wananchi kuendelea kudumisha amani, umoja na mshikamano, akibainisha kuwa CCM imekuwa chama kinachoweka mbele maslahi ya wananchi wote bila kujali itikadi.
“Tunachagua maendeleo, CCM ni chaguo sahihi!” alisisitiza Katele .
Katele aliwaahidi wakazi wa Pangani kuwa endapo watampa ridhaa ya kuendelea kuongoza, ataendelea kusimamia utekelezaji wa miradi ya maji, elimu, afya na barabara, akisema dhamira yake ni kuhakikisha kila mwananchi ananufaika na matunda ya maendeleo.




