Wananchi wa kata ya Kakesio iliyoko Tarafa ya Ngorongoro Wilaya ya Ngorongoro Mkoani Arusha watanufaika na mradi wa Maji kwa ajili ya Mifugo na matumizi ya binadamu kufuatia Serikali kupitia Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) kuchimba Kisima cha Maji chenye urefu wa mita 110 ambacho kinatarajiwa kuzalisha maji lita 80,000 kwa siku.
Uchimbaji wa Kisima hicho ni muendelezo wa kazi nzuri inayofanya na Serikali kwa Wananchi wanaoishi katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro ambapo Kisima kama hicho kimechimbwa eneo la Mlima matiti kwa ajili ya wananchi wa Kata ya Endulen na Alaetoli na baadae mradi kama huo utatekelezwa katika Kata ya Olbalbal ili kusaidia wananchi kukabiliana na changamoto ya upungufu wa maji kwa mifugo katika msimu wote wa mwaka.




