Katikati ni mkuu wa mkoa wa Rukwa Makongoro Charles Nyerere wakati akiwahimiza wananchi kujitokeza siku ya tarehe 29 kupiga kura na kuwachagua viongozi wanaowataka. 
Mkuu wa mkoa wa Rukwa Makongoro Nyerere akiwa katika gari la kubebea wagonjwa alilolikabidhi kwa jeshi la zimamoto na uokoaji leo
Na
Neema Mtuka, Sumbawanga
Rukwa:Mkuu wa mkoa wa Rukwa Makongoro Charles Nyerere amewataka wananchi kushiriki katika uchaguzi mkuu utakaofanyika oktoba 29 mwaka.
Akizungumza leo Oktoba 27 ,2025 wakati akikabidhi magari matatu kwa jeshi la zimamoto na uokoaji Makongoro ameitangaza siku hiyo kuwa siku ya mapumziko ya kitaifa ili watanzania wote wapate nafasi ya kushiriki kikamilifu katika zoezi la upigaji wa kura.
“Uchaguzi ni chachu ya maendeleo,si chanzo cha mgawanyiko ,baada ya uchaguzi tuendelee kuwa wamoja kama watanzania”amesema Makongoro.
Kwa mujibu wa ibara ya 5 ya katiba ya jamhuri ya muungano wa Tanzania (1977) na Sheria ya uchaguzi ya mwaka 2024 kila raia mwenye sifa ana haki na wajibu wa kushiriki katika uchaguzi mkuu utakaofanyika oktoba 29 mwaka huu.
Aidha amesema zikiwa zimebaki siku mbili watanzania kupiga kura amewataka wajitokeze na kuwachagua Rais ,wabunge na madiwani kwa lengo la kujiletea maendeleo kwenye maeneo yao.
Sambamba na hilo pia amewasisitiza wananchi kuwa uchaguzi utakuwa huru na hali ya usalama katika mkoa wa Rukwa ni shwari,na itaendelea kuwa thabiti kabla ,wakati na baada ya uchaguzi.
Ameongeza kuwa vyombo vya ulinzi na usalama vimejipanga kikamilifu kuhakikisha kuwa wananchi wote wanashiriki kupiga kura katika mazingira ya amani,utulivu na usalama wa hali ya juu.
” Wananchi msiogope,mjitokeze kwa wingi kwani serikali imechukua hatua zote muhimu za kuhakikisha kuwa kila kituo cha kupigia kura kinakuwa salama na kila mwananchi anatekeleza haki yake ya kikatiba bila hofu wala wasiwasi.” Amesisitiza Makongoro



