Katikati ni mkuu wa mkoa wa Rukwa Makongoro Charles Nyerere wakati akikata utepe na kukabidhi magari matatu kwa Jeshi la zimamoto na uokoaji
Mkuu wa mkoa wa Rukwa wakati akikata utepe na kukabidhi magari matatu ya kisasa kwa jeshi la zimamoto na uokoaji.
…………….
Na Neema Mtuka, Sumbawanga
Rukwa:Mkuu wa mkoa wa Rukwa Makongoro Charles Nyerere amekabidhi magari matatu ya kisasa kwa jeshi la zimamoto na uokoaji kwa ajili ya kuweza kusaidia kuokoa maisha ya watu na mali zao.
Akizungumza leo Oktoba 27,2025 katika hafla fupi ya makabidhiano katika uwanja wa ofisi ya mkuu wa mkoa wa Rukwa Makongoro amewataka kutumia magari hayo kwenye matumizi yaliyokusudiwa na kuacha tabia ya kuiba mafuta.
“Natoa wito kwa jeshi la zimamoto kutunza magari hayo na kuyatumia ipasavyo katika shughuli za uokoaji na si vinginevyo” amesema Makongoro
Amesema hayo ni magari ya awali na mengine Dkt Samia ameyaagiza na kila wilaya itapata gari moja kubwa la kisasa kwa ajili ya uokoaji
“Kupatikana kwa magari haya kutapunguza changamoto ya kuchelewa kufika kwenye matukio na kuokoa maisha na mali za watu”amesema
Amewataka kutumia magari hayo kwa shughuli inayokusudiwa na kwa kufuata utaratibu uliowekwa kwa mujibu wa sheria na kuwa waadilifu hasa kwa matumizi ya mafuta .
Ametoa wito wa kila halmashauri kutenga maeneo ya kujenga kituo cha zimamoto ili wananchi wapate huduma kwa haraka.
“Magari haya ni mali ya umma hivyo kila mmoja anapaswa kuyatuñza kama ya kwake.” Amesisitiza Makongoro
Kwa upande wake mkaguzi msaidizi wa jeshi la zimamoto na uokoaji Mkoa wa Rukwa Brian John amesema ujio wa magari hayo matatu utarahisisha upatikanaji wa huduma bora katika uokoaji na wataweza kuwafikia wananchi kwa wakati.
Ameongeza kuwa magari hayo yatatumika kama inavotakiwa kwa kuwa jeshi la zimamoto na uokoaji lina askari waliopatiwa mafunzo ndani na nje ya nchi ,ambao wamepata mafunzo ya majini ,uzimaji wa moto na katika majanga mengine pindi yanapotokea na wanatumia vifaa vya kisasa vya kidigitali.
Amewataka wananchi kupiga simu bure pindi matukio ya moto na majanga mengine yanapotokea ili kuweza kuokoa maisha na mali zao na wataendelea kutoa elimu juu ya majanga mbalimbali ikiwemo ya moto.
Nao baadhi ya wananchi akiwemo Benjamin Masawe mkazi wa Katandala manispaa ya Sumbawanga amesema kuwa vifaa hivyo vitasaidia kupunguza malalamiko kwa wananchi ambao wamekuwa wakihoji kuhusu magari hayo kukosa maji wakati majanga yakiwa yametokea.




