Na.Meleka Kulwa- Dodoma
WIZARA ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imetoa tuzo kwa wanafunzi ambao ni washindi wa uandishi wa insha kwa Nchi za Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kwa mwaka 2023 na 2024 huku ikiwasisitiza kutumia uwezo wao binafsi katika kuandika insha badala ya kutegemea matumizi ya teknolojia ya Akili Mnemba.
Akizungumza katika hafla ya utoaji tuzo hizo leo Oktoba 26,2025 jijini Dodoma Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt.Hussein Omar amesema kuwa uandishi wa insha ni sehemu ya mafunzo na inawajengea wigo mpana wa kujifunza masuala muhimu yanayohusu jumuiya hizo.
“Nawaomba wanafunzi kujiepusha na matumizi ya Akili Mnemba katika kuandika insha zenu kwa sababu kwanza itakuwa sio uhalisia wa uandishi wenu, lakini pia ni aina ya udanganyifu ambao utawatoa kwenye kinyang’anyiro cha ushindani,” amesema Dkt.Omar
Aidha, amewataka wanafunzi kutumia teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) kwa ufasaha katika kufanya tafiti ili kuongeza maarifa kuhusu shughuli, malengo na mipango ya jumuiya hizo mbili.
Aidha amesema kuwa ushindi huo ni ishara ya ubora wa elimu nchini na juhudi za pamoja za walimu, wakuu wa shule, na wizara husika katika kuandaa wanafunzi wenye uwezo mkubwa wa kufikiri na kujenga hoja.
“Ninafarijika kuona wanafunzi wetu wanaongoza katika ngazi za kikanda, jambo linaloonyesha kuwa Tanzania inaendelea kufanya vizuri katika kukuza elimu bora na ubunifu kwa vijana wake,” amesema
Pia ametoa wito kwa wakuu wa shule na waratibu wa insha kuhakikisha wanafunzi wote wanashiriki kikamilifu katika mashindano hayo kwa kufuata miongozo iliyowekwa, huku akisisitiza umuhimu wa kuhamasisha wanafunzi wenye mahitaji maalumu kushiriki.
“Wakuu wa shule ni wasimamizi wakuu wa mashindano hayo, hivyo wanapaswa kuhakikisha wanafunzi wanashiriki kikamilifu na kufuata taratibu za uandishi ili kuepuka kuondolewa katika hatua za usahihishaji,” ameongeza Dkt.Omar
Kwa upande wake Kamishna wa Elimu, Dkt. Lyabwene M. Mtahabwa,amesema mashindano hayo yamekuwa kichocheo kikubwa cha kukuza umahiri wa wanafunzi katika uandishi, utafiti, na ufahamu mpana wa masuala ya kijamii, kiuchumi na kisiasa katika jumuiya hizo mbili za kikanda.
“Mashindano hayo yamekuwa chachu kwa vijana kufanya utafiti, kujifunza na kuelewa vyema hatua za uimarishaji mahusiano baina ya nchi wanachama na umuhimu wa muunganiko huu wa kikanda,” amesema Dkt. Mtahabwa.
Dkt. Mtahabwa amewapongeza washindi wote wa kitaifa na kikanda, akiwemo Hollo Alice Kadala kutoka Shule ya Sekondari Msalato, aliyeshika nafasi ya tatu kitaifa na ya tatu kikanda katika mashindano ya SADC mwaka 2023, pamoja na Blandina Kabalemesa wa Shule ya Sekondari Anwarite, aliyeshika nafasi ya kwanza kitaifa na ya nne kikanda katika mashindano ya EAC mwaka 2024.
“Hawa wanafunzi ni mfano bora wa kuigwa. Ushindi wao unaonyesha juhudi na ubora wa elimu yetu. Tunawapongeza walimu, wazazi na waratibu wote kwa malezi bora na mwongozo uliowezesha mafanikio haya,” amesema
Awali, Mratibu wa Insha kutoka Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia Bi.Matuha Masati,ameipongeza Sekretarieti ya Afrika Mashariki na Jumuiya ya Nchi za SADC Kwa kuendesha Mashindano ya Uandishi wa Insha kwani yamekuwa chachu Kwa vijana kufanya utafiti,kujifunza na kufahamu vizuri mchakato na hatua mbalimbali za uimarishaji Kwa nchi wanachama.
Amesema kuwa mashindano hayo husimamiwa na Baraza la Taifa la Mitihani (NECTA) kwa insha za nchi za Afrika Mashariki (EAC) na za SADC husimamiwa na Wizara ya Elimu kwa upande wa Tanzania bara na Zanzibar.
Amesema kuwa jumla ya wanafunzi 1,096 walishiriki katika mashindano ya uandishi wa insha za EAC na SADC mwaka 2023, wakiwemo wanafunzi 557 wa EAC na 539 wa SADC, huku mwaka 2024 ukishirikisha wanafunzi 892, kati yao 243 wa SADC na 649 wa EAC.
“Kwa sasa, Wizara inatoa tuzo kwa washindi 10 bora wa kitaifa kwa kila shindano, tofauti na ilivyokuwa awali ambapo walipewa tu washindi watatu wa juu. Hatua hii imeongeza hamasa kubwa kwa wanafunzi kushiriki,” amesema




