…………
Imeelezwa kuwa uwepo wa wataalamu wa Manunuzi na Ugavi waliopatiwa mafunzo ya ziada na kusajiliwa na Bodi ya PSPTB utasaidia katika tasnia ya ukaguzi wa mnyororo wa ugavi. Hatua hiyo itaiwezesha Bodi kuongeza tija na kubaini mapungufu yanayojitokeza ili yaweze kurekebishwa na kufanya mfumo huo kuwa imara zaidi.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Bi. Jenifa Omolo, wakati akitoa hotuba katika mahafali ya 14 ya Bodi ya PSPTB yaliyofanyika leo, Oktoba 24, katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.
Aidha, ametoa rai kwa makampuni ya ukaguzi kuona umuhimu wa kuwaajiri wataalamu wa manunuzi na ugavi ili kusaidia katika utekelezaji wa majukumu yao ya ukaguzi. Alisema:
“Natambua kuwa kwa muda sasa kumekuwepo na baadhi ya waajiri wanaofumbia macho mchango wa fani hii. Hali hiyo inatoa mwanya kwa watu wengine kufanya kazi za ununuzi na ugavi bila kutimiza vigezo vya kitaaluma.”
Vilevile, amewataka wahitimu kufanya kazi kwa uadilifu na weledi, akibainisha kuwa kufanya kazi ya ununuzi na ugavi bila taaluma husika ni ukiukwaji wa Sheria ya PSPTB Na. 23 ya mwaka 2007.
Bi. Omolo, kupitia mahafali hayo, ameelekeza waajiri wote wa sekta ya umma na binafsi nchini kuzingatia matakwa ya kifungu cha 11 cha sheria hiyo, ambacho kimeweka adhabu kwa wote watakaobainika kukiuka masharti yake.
Pia ameiagiza Bodi kuendelea kusimamia utekelezaji wa sheria hiyo kwa kufanya ukaguzi katika sekta za umma na binafsi, na kuwabaini wote wanaoendelea kufanya kazi za manunuzi na ugavi bila kuwa na sifa stahiki za kitaaluma. Alisema:
“Tutalitazama hili kwa makini. Bila kufaulu mitihani ya Bodi, huwezi kupanda cheo. Zamani, bila kuwa na CPA huwezi kuwa Mhasibu; vivyo hivyo, bila taaluma hii huwezi kuwa Afisa Manunuzi.”
Aidha, ameiagiza Bodi, kupitia Kamishna wa Sera na Ununuzi katika Wizara ya Fedha, kukutana ili kushughulikia maslahi ya wataalamu wa kada ya ununuzi na ugavi.
Pia amesisitiza kuwa wakurugenzi, wakuu wa idara na wataalamu wa vitengo vya ununuzi na ugavi wawe ni wale wenye sifa zinazotambulika kisheria kwa mujibu wa Sheria ya PSPTB ya mwaka 2007 na Waraka wa Hazina Na. 3 wa mwaka 2015.
Hata hivyo, amewahimiza wahitimu hao kuendelea kujifunza katika vyuo mbalimbali duniani ili kukuza taaluma zao na kujiandaa kwa ushindani wa soko la ajira la kimataifa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya PSPTB, Bw. Jacob Kibona, ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Fedha kwa kuwapatia jumla ya shilingi milioni 900 kwa ajili ya kutekeleza majukumu ya Bodi. Amesema fedha hizo zimeiwezesha Bodi kufanikisha ukaguzi katika zaidi ya taasisi 300 za Serikali.
Katika hatua nyingine, Mwenyekiti huyo alimwomba mgeni rasmi kuipatia ofisi Bodi hiyo ili iweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi — ombi ambalo limekubaliwa na Naibu Katibu Mkuu, aliyekiri kuwa atalifanyia kazi haraka iwezekanavyo.
Naye Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel, amewakumbusha wahitimu kuwa mafanikio kazini hayataegemea vyeti walivyopata, bali namna watakavyovitendea haki kwa kufanya kazi kwa uaminifu na weledi. Amesema kuwa vyeti vitakuwa havina maana endapo wahitimu hao watakiuka misingi ya maadili na uwajibikaji.






