NA JOHN BUKUKU -ZANZIBAR
Aliyekuwa Mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Ziwa Victoria, Ezekiel Wenje, amesema kuwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimegoma kushiriki Uchaguzi Mkuu kwa sababu hakikuwa na maandalizi na fedha ambazo zingekiwezesha kushiriki uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025.
Ameyasema hayo Oktoba 24, 2025 katika viwanja vya Mnazi Mmoja, Zanzibar, katika muendelezo wa kampeni za Mgombea Urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Amesema kuwa Mgombea Urais wa CHADEMA hakuwa na pesa ambazo zingemwezesha kufanya mikutano yake ya kampeni.
Aidha, amebainisha kuwa CHADEMA kiliamua chenyewe kugomea uchaguzi pasipo kushinikizwa na mtu yeyote, kutokana na kukosa rasilimali fedha za kuendesha mikutano ya kampeni, ndipo kilipoamua kuja na kauli mbiu ya “No Reforms, No Election.”
Amesema kuwa kila mmoja anajua kuwa kabla ya uongozi wa sasa haujaingia madarakani, hakukuwa na mikutano ya hadhara wala maandamano kwa vyama vya upinzani.
Aidha, amebainisha kuwa Dkt. Samia alipoingia madarakani aliruhusu watu kuanza kuandamana na pia amefuta kesi ambazo zilikuwa zinawakabili viongozi wa CHADEMA.
Amesema kuwa Dkt. Samia alipoingia madarakani aliweza kuwaruhusu na kuwarejesha nchini wale waliokuwa wameikimbia nchi baada ya uchaguzi wa mwaka 2020.
Aidha, amesema kuwa chini ya uongozi wa Dkt. Samia, serikali imefanya uwekezaji mkubwa kwa kuwaleta wawekezaji kuwekeza nchini, ikiwemo katika bandari ya Bagamoyo, akibainisha kuwa uwekezaji huo una tija kwa taifa.
Aidha, amebainisha kuwa katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Dkt. Samia, Tanzania Bara imepiga hatua kubwa ya kimaendeleo na serikali nzima ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.




