Mgombea wa nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa Ndugu Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza na wananchi wa Zanzibar katika muendelezo wa Kampeni za Uchaguzi za CCM zilizofanyika katika viwanja vya Mnazi mmoja, Mkoa wa Mjini Magharibi tarehe 24 Oktoba, 2025.
Mgombea Urais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi.
………………..
NA JOHN BUKUKU , ZANZIBAR
Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema ataendelea kushirikiana kwa karibu na Mgombea Urais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, kulinda na kuimarisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa manufaa ya Watanzania wote.
Amesema Muungano ni alama ya umoja, amani na maendeleo, hivyo yeye na Dkt. Mwinyi wataendelea kuudumisha kwa vitendo ili kuhakikisha unaendelea kuwa imara, wenye manufaa kwa pande zote mbili za Muungano.
“Tutashirikiana bega kwa bega kuhakikisha Muungano wetu unazidi kuwa imara, unaolinda maslahi ya Watanzania na kuleta maendeleo endelevu kwa Taifa letu,” alisema Dkt. Samia.
Aidha, Dkt. Samia ametoa wito kwa Watanzania wote wenye sifa kujitokeza kwa wingi kupiga kura Oktoba 29 mwaka huu, akisema kufanya hivyo ni njia bora ya kuchagua viongozi watakaolinda amani na kuendeleza mafanikio yaliyopatikana.
Amesisitiza kuwa wananchi hawapaswi kuwa na hofu yoyote, kwani vyombo vya ulinzi na usalama vipo kazini kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani, usalama na utulivu katika maeneo yote ya nchi.
“Naomba Watanzania wote mjitokeze kwa wingi kupiga kura kwa amani na utulivu. Vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vimejipanga kuhakikisha kila raia anatekeleza haki yake ya kikatiba bila wasiwasi,” alisisitiza Dkt. Samia.
Baada ya kuhitimisha kampeni za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa upande wa Zanzibar, sasa uelekeo wa CCM ni jijini Mwanza, ambako chama hicho kinatarajiwa kufunga rasmi kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2025.











