*Amesema atakayefanya hivyo sheria inaruhusu ashughulikiwe
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira amesema moja ya sharti la haki za binadamu ni kutowazuia wengine kupata haki yao ya kikatiba ikiwemo kupiga kura kuchagua viongozi na watakaodanya hivyo hawatavumiliwa.
Amesema CCM inaheshimu haki za binadamu, lakini atakayeshindwa kuziheshimu na kusababisha uvunjifu wa sheria, atashughulikiwa kwa kadri sheria inavyoelekeza.
Aidha, amewahakikishia Watanzania kwamba kila mwenye sifa atapata fursa ya kupiga kura kwa amani na utulivu na kwamba hakuna yeyote atakayezuia uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, mwaka huu kumchagua rais, wabunge na madiwani.
Wasira ameema hayo leo Oktoba 24, 2025 alipokuwa akizungumza na wana CCM wilayani Bukoba, Mkoa wa Kagera akiwa katika ziara ya kumnadi mgombea urais wa CCM Dk. Samia Suluhu Hassa, wagombea ubunge na udiwani waliosimamishwa na Chama.
“Wenye matatizo madogomadogo sisi tunawaambia wanazungumza sana haki za binadamu na sisi tunawaambia tunaziheshimu, lakini haki za binadamu zina masharti na masharti yake ni kwamba kama unadai haki yako wewe usiwazuie wengine kupata haki zao,” alisema.
Amesema kuwa, Mgombea urais kupitia CCM Dk. Samia ameahidi ndani ya siku 100 baada ya uchaguzi wa mwaka huu ataanza kukaa pamoja na wanaohitaji kuzungumza naye juu ya mambo wanayoona hayako sawa.
“Sisi hatujakataa kusikiliza hata kidogo, Dk. Samia amesema katika siku zake 100 baada ya uchaguzi ataanza mjadala na wale ambao wanahitaji kuzungumza naye, maana hatuendeshi nchi kwa mabavu tunaendesha kwa mazungumzo.
“Kwa hiyo kama kuna mmoja anafikiri yeye ana mawazo lakini hayajasikilizwa bado nafasi ya kusikilizwa ipo, huwezi kusema utafanya fujo kwa sababu hujasikilizwa, utashughulikiwa kwa sababu kuna kusikilizwa lakini kama hutaki kusikilizwa unashughulikiwa ili walio wengi wapate amani maana ni haki yao kupiga kura.
“Sheria zipo zinasema watu wakienda kupiga kura hakuna anayeruhusiwa kuwashawishi kimyakimya au hata waziwazi kwamba wasiende kupiga kura, anaingilia haki yao,” ameeleza.




