
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi (TISEZA) Bw. Gilead Teri, akizungumza katika kikao kazi na wahariri wa vyombo vya habari kilichofanyika leo, Oktoba 23, 2025, jijini Dar es Salaam.

Makamu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Bw. Bakari Machumu akizungumza katika kikao kazi na Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi (TISEZA) kilichofanyika leo, Oktoba 23, 2025, jijini Dar es Salaam.


……
Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi (TISEZA) imepanga kuhakikisha ifikapo mwaka 2026 inasajili miradi 1,500 ya uwekezaji yenye thamani isiyopungua dola za Kimarekani bilioni 15, sambamba na kuhakikisha Tanzania inakuwa kinara wa uchumi katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Akizungumza katika kikao kazi na wahariri wa vyombo vya habari kilichofanyika leo, Oktoba 23, 2025, jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa TISEZA, Bw. Gilead Teri, amesema uwekezaji una manufaa mengi ikiwemo kuongeza mitaji, ajira, mapato ya kodi, pamoja na kuleta teknolojia mpya na za kisasa katika uchumi wa nchi.
Bw. Teri ameongeza kuwa mamlaka hiyo inalenga pia kuongeza mauzo ya bidhaa nje ya nchi, hatua itakayowanufaisha moja kwa moja wawekezaji, makampuni na Taifa kwa ujumla.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa wahariri wa vyombo vya habari katika kuhabarisha umma kuhusu mageuzi ya kiuchumi yanayoendelea chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
“Tunaendelea kuandaa uzinduzi wa huduma katika eneo maalum la kiuchumi la Ubungo, ambapo tutatoa huduma bure kwa Watanzania wanaotaka kuuza bidhaa zao nje ya nchi na kujifunza namna ya kuagiza mitambo kwa ajili ya kuanzisha viwanda,” amesema Bw. Teri.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Bw. Bakari Machumu, ameipongeza TISEZA kwa hatua ya kuwaelimisha wahariri kuhusu utekelezaji wa majukumu yake na sheria mpya ya uwekezaji.
Amesema kuwa elimu hiyo itawasaidia wahariri kuelewa vyema masuala ya uwekezaji, kuandika kwa weledi, na kutoa taarifa zitakazosaidia watunga sera na taasisi husika kufanya maboresho pale panapohitajika.
“Kikao hiki kimetupa uelewa mpana kuhusu TISEZA na sheria mpya ya uwekezaji. Hii itatuwezesha kuandika kwa usahihi, kuuliza maswali sahihi, na kuchochea maboresho katika sekta ya uwekezaji nchini” amesema.



