Na.Sophia Kingimali.
Wakati Watanzania wakijiandaa kushiriki katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025, muunganiko wa asasi za kiraia zinazotetea makundi maalum, ikiwemo wanawake, watoto na vijana wanawake zimeitaka Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), vyama vya siasa na wadau wote kuhakikisha mazingira ya uchaguzi yanabaki kuwa salama, huru na jumuishi, bila vitisho au ukatili wa kijinsia unaoweza kuwakwamisha wanawake.
Akisoma Tamko liliandaliwa na asasi hizo leo Octoba 23,2025 Jijini Dar es salaam Muasisi na muanzikishi wa Chama cha Waandishi wa habari wanawake (TAMWA) Rose Mwalimu amesema ushiriki wa wanawake ni nguzo muhimu ya demokrasia jumuishi na maendeleo endelevu. “Tunaamini kwamba pale viongozi wanawake wanapopata nafasi ya uongozi, hatua mahsusi za kuinua kipato na maisha ya wanawake zinawezekana zaidi,” amesema bi.Mwalimu.
Aidha Asasi hizo zimewahimiza wanawake kote nchini kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura huku wakisisitiza kuwa kushiriki uchaguzi ni kutekeleza wajibu wa kikatiba. “Tunapokwenda kuchagua viongozi wetu, tuhakikishe tunawapa dhamana wale watakaosimamia ajenda za maendeleo ya wanawake, watoto, na vijana,” Amesisitiza.
Ameongeza kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi za Afrika zilizoonesha maendeleo katika ushiriki wa wanawake kwenye siasa, huku wakimtaja Rais Samia Suluhu Hassan kama mfano wa mafanikio ya mwanamke kiongozi.
“Kwa mara ya kwanza tumeshuhudia wanawake kadhaa wakigombea urais na nafasi nyingine za juu, jambo linaloonesha ukuaji wa demokrasia yetu,” limeeleza tamko hilo.
Miongoni mwa wagombea wanawake wa urais mwaka huu ni Saumu Rashid wa UDP, Mwajuma Mirambo wa UMD, huku wagombea wenza wanawake wakiwa ni pamoja na Eveline Munis (NCCR), Husna Mohamed (CUF), Aziza Haji (Demokrasia Makini), Amani Selemani (TLP), Chausiku Mohamed (NLD), Sakia Mussa (SAU), na Devotha Minja (CHAUMA).
“Asasi hizi zinatoa rai kwa wananchi kutohukumu viongozi wanawake kwa misingi ya jinsia bali kwa uwezo na dira yao ya maendeleo Uongozi wa mwanamke si tishio, bali ni chachu ya kuimarisha demokrasia jumuishi yenye kusikiliza na kutenda kwa manufaa ya wote.”
Aidha, asasi hizo zimekemea vikali matamshi ya kejeli, udhalilishaji na mashambulizi ya kibinafsi kwa wagombea wanawake, zikisema ni wakati wa mjadala wa sera na hoja zenye kujenga taifa.
“Wanawake wanaogombea nafasi mbalimbali wasibezwe wala kudhalilishwa kwa maneno yenye misingi ya kijinsia kwani kupatikana kwa Rais mwanamke kumesaidia nchi kusonga mbele katika utekelezaji wa Dira ya Maendeleo Endelevu (SDG 5) inayohusu usawa wa kijinsia. Kupitia uongozi wa Rais Samia, tumeshuhudia mageuzi katika sheria za kisiasa na miradi mikubwa ya maendeleo,” wamesema.
Sambamba na hayo bi Mwalimu amemezitaka taasisi za habari nchini kuhakikisha zinatoa fursa sawa kwa wagombea wanawake kushiriki midahalo na vipindi vya mijadala ili kuongeza uelewa wa umma kuhusu mchango wa wanawake katika maendeleo.
Aidha bi Mwalimu amehitimisha kwa kusisitiza kuwa uongozi bora hauna jinsia, bali unategemea maadili, dira, na dhamira ya kuwahudumia wananchi wote kwa usawa.
“Tanzania ni yetu sote, wanaume kwa wanawake, na maendeleo ya kweli yatapatikana tu pale ambapo usawa wa kijinsia utawekwa mbele,” Amesema.