NA JOHN BUKUKU- DAR ES SALAAM
Baada ya kufanya mkutano mkubwa wa kampeni katika eneo la Kinyerezi, Wilaya ya Ilala jana, Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo anaendelea na kampeni zake jijini Dar es Salaam kupitia mkutano wa hadhara unaofanyika Buza Tanesco, Wilaya ya Temeke.
Wananchi wa Temeke na maeneo jirani wameonekana wakiwa katika hali ya furaha na hamasa kubwa wakijiandaa kumpokea Dkt. Samia, huku wakiwa wamepambwa kwa bendera na mavazi ya kijani na njano ya CCM.
Kwa mujibu wa viongozi wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, mkutano wa leo unatarajiwa kuvutia maelfu ya wananchi, ukiwa ni mwendelezo wa kampeni zinazolenga kueleza utekelezaji wa Ilani ya Chama na dira ya maendeleo endelevu ya Serikali ya Awamu ya Sita.
Katika mkutano huo, Dkt. Samia anatarajiwa kuelezea mafanikio yaliyopatikana katika sekta za miundombinu, elimu, afya, ajira kwa vijana, uwezeshaji wa wanawake, na huduma za jamii, sambamba na kuainisha mikakati mipya kwa kipindi kijacho.
Aidha, anatarajiwa kuhimiza Watanzania wote kujitokeza kwa wingi kupiga kura Oktoba 29 kwa amani na utulivu, na baada ya kupiga kura warudi majumbani kwa utulivu kusubiri matokeo, ili kulinda heshima na umoja wa taifa.