NA JOHN BUKUKU – KINYEREZI
Kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Bw. Peter Msigwa, amemwelezea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuwa ni kiongozi mwenye maono makubwa aliyefanikisha mageuzi ya maendeleo katika sekta mbalimbali nchini. Msigwa alikuwa akihutubia katika mkutano wa kampeni uliofanyika kwenye uwanja wa Kecha, Kinyerezi, wilayani Ilala, jijini Dar es Salaam.
Katika hotuba yake, Msigwa alieleza kuwa Dkt. Samia amedhihirisha dhamira ya dhati ya kuyaenzi mazuri ya watangulizi wake, kama alivyoahidi wakati wa hotuba yake ya kwanza bungeni baada ya kuapishwa kuwa Rais. “Alisema wazi kuwa atayaenzi mema yote ya watangulizi wake, na kwa hakika ameyatekeleza kwa vitendo,” alisema Msigwa.
Akiwa kama kada aliyefanya ziara katika maeneo mbalimbali ya Tanzania, Msigwa alisema kila mahali alikopita alishuhudia mabadiliko makubwa yaliyochochewa na uongozi wa Dkt. Samia. “Katika sekta ya maji, afya, elimu, barabara na nishati, sura ya Rais Samia inaonekana. Tulidhani miradi mikubwa 17 aliyoirithi isingewezekana, lakini ametuvusha,” alisisitiza.
Akizungumzia juhudi za serikali katika sekta ya kilimo, Msigwa alisema kuwa Rais Samia amechukua hatua madhubuti kuwekeza kwenye kilimo kama uti wa mgongo wa uchumi. Alitaja ongezeko la upatikanaji wa mbolea kutoka tani laki tatu hadi zaidi ya tani milioni moja na laki mbili kuwa ni ishara ya dhamira ya dhati ya Rais Samia katika kulijenga Taifa kupitia kilimo.
Aidha, Msigwa aliweka msisitizo kuhusu umuhimu wa utulivu wa kisiasa nchini na kuhimiza vijana kutokubali kutumika kuvuruga amani. “Mabadiliko ni mchakato. Tunahitaji kiongozi mwenye utulivu. Tanzania ya sasa ina utulivu wa kisiasa, kiuchumi na kijamii. Vijana, tusichome vijiji, bali tukajitokeze kwa wingi kupiga kura,” alisema.
Msigwa aliwaomba Watanzania, hususan vijana, kujitokeza kwa wingi katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, na kumpa kura ya ndiyo Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ili aendelee kuiongoza Tanzania katika njia ya maendeleo na ustawi wa wananchi wote.