Mgombea wa nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa Ndugu Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza na wananchi wa majimbo ya Ilala, Segerea, Kivule na Ukonga katika muendelezo wa Kampeni za Uchaguzi za CCM zilizofanyika kwenye uwanja wa Kecha, Kinyerezi Jijini Dar es Salaam tarehe 22 Oktoba, 2025.
Mgombea wa nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa Ndugu Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwakabidhi Ilani ya Uchaguzi baadhi ya wagombea Ubunge wa Majimbo mbalimbali ya Mkoa wa Dar es Salaam katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Kecha Kinyerezi Jijini Dar es Salaam tarehe 22 Oktoba, 2025.

………….
NA JOHN BUKUKU -KINYEREZI
Oktoba 22, 2025
Mgombea Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameahidi kutekeleza miradi mikubwa katika Wilaya ya Ilala itakayochochea shughuli za kiuchumi na biashara, ikiwemo ujenzi wa Daraja la Jangwani lenye urefu wa mita 390, ujenzi wa barabara za juu Tabata, Buguruni na Faya, pamoja na ujenzi wa soko kubwa la machinga na wafanyabiashara wadogo eneo la Jangwani.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika katika Wilaya ya Ilala, Dkt. Samia alisema kuwa katika miaka mitano ijayo Serikali ya CCM itatekeleza miradi muhimu itakayoongeza fursa nyingi za kibiashara na kiuchumi kwa wakazi wa Ilala na maeneo ya jirani.
Alisema katika kipindi cha miaka mitano iliyopita Serikali imefanya maendeleo makubwa ndani ya Wilaya ya Ilala, ikiwemo kukamilisha machinjio ya kisasa ya Vingunguti, ujenzi wa masoko 10 ya kisasa, na maboresho ya Soko Kuu la Kariakoo.
Dkt. Samia aliongeza kuwa ongezeko la utolewaji wa leseni za biashara ni ishara kuwa biashara zimeendelea kukua kutokana na mazingira bora ya uwekezaji yanayowekwa na Serikali.
Aidha, baadhi ya makada na wagombea ubunge wa CCM katika Mkoa wa Dar es Salaam walisema uwekezaji mkubwa uliofanyika katika Bandari ya Dar es Salaam umeongeza ufanisi wa utendaji, na kusaidia kuharakisha usafiri na usafirishaji wa shehena za mizigo kwenda maeneo mbalimbali ya nchi.
Mgombea Ubunge wa Jimbo la Ilala kupitia CCM, Mussa Zungu, alisema Serikali ya awamu ya sita imeleta mapinduzi makubwa katika sekta ya miundombinu na kwamba utekelezaji wa miradi mipya utaleta ajira na kuinua biashara za wananchi.
Naye Mgombea Ubunge wa Jimbo la Arusha Mjini kupitia CCM, Paul Makonda, alisema kuwa miradi inayopangwa na Serikali ya CCM ni ishara ya maendeleo ya kweli na utekelezaji wa ahadi kwa vitendo, huku akisisitiza umuhimu wa wananchi kuendelea kuiamini CCM.
Kwa upande wake, Mgombea Ubunge wa Jimbo la Segerea, Bona Kamoli, alisema Ilani ya CCM ya mwaka 2025–2030 imebeba dira ya maendeleo ya Watanzania kwa kuzingatia mahitaji ya wananchi katika sekta zote.
Wakati huo huo, Aliyekuwa Mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Kusini, Aden Mayala, ametangaza kujiunga na CCM, akisema chama hicho kimeonyesha kuwa na mipango na dhamira ya kweli ya kuwatumikia Watanzania.
Akizungumzia hatua hiyo, Dkt. Samia alisema CCM itaendelea kuimarisha umoja wa kitaifa na kuhakikisha kila Mtanzania ananufaika na rasilimali za nchi kupitia miradi endelevu inayotekelezwa na Serikali.
Ifahamike kuwa Alhamisi hii, Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuhitimisha kampeni zake za kuomba kura ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam kwa kufanya mikutano katika majimbo ya Temeke na Kigamboni.




