NA JOHN BUKUKU- DAR ES SALAAM
Waziri wa Ujenzi, Mhe. Abdallah Ulega, amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa ya kizalendo anayofanya kuwaletea wananchi maendeleo. Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika katika viwanja vya Leaders Club, Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam, Ulega alisema kuwa ndani ya miaka minne ya uongozi wa Dkt. Samia, kiasi cha shilingi trilioni 1.7 kimetumika kubadilisha sura ya Jiji la Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Waziri Ulega, fedha hizo nyingi zimeelekezwa kwenye ujenzi wa miundombinu, barabara, madaraja na mifereji ya maji taka, hatua ambayo imeleta unafuu mkubwa kwa wakazi wa jiji hilo. Alisisitiza kuwa maendeleo hayo yamewezesha kupungua kwa msongamano barabarani na kudhibiti mafuriko ambayo kwa muda mrefu yamekuwa tatizo kubwa.
“Trilioni moja nukta saba ni fedha nyingi sana. Tumezielekeza kwenye vipaumbele vya jiji letu: kupunguza msongamano wa magari, ujenzi wa madaraja, barabara pana, na mifereji ya kisasa ya kupitisha maji. Dkt. Samia amelifanyia kazi jiji hili kwa namna ya kipekee,” alisema Ulega.
Akiainisha baadhi ya miradi hiyo, Waziri Ulega alitaja ujenzi wa daraja refu lenye urefu wa mita 400 lililojengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 27. Alisema daraja hilo limejengwa katika eneo lililokuwa na changamoto kubwa ya mafuriko, na kwamba sasa wananchi wanafanya shughuli zao kwa uhuru bila bughudha.
Aidha, Ulega alibainisha kuwa mafanikio ya Rais Samia katika ujenzi wa miundombinu yamevuka mipaka, ambapo hata Benki ya Dunia kupitia Mkurugenzi wake wa Kanda ya Afrika imetambua kasi ya maendeleo ya Tanzania, hasa katika ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara. Alisisitiza kuwa hiyo ni sababu tosha kwa Watanzania kujitokeza kwa wingi Oktoba 29 na kumpigia kura Rais Samia Suluhu Hassan.
Kwa upande mwingine, alieleza kuwa Serikali imetoa shilingi bilioni 17 kwa ajili ya kudhibiti mafuriko kutoka Magomeni hadi Mkwajuni, na kiasi cha bilioni 11 kwa ajili ya daraja kutoka Kigogo hadi Karume. Miradi mingine iko Kunduchi hadi Ununio, yote ikiwa ni juhudi za kuimarisha mazingira ya jiji.
Akihitimisha, Waziri Ulega alisema kuwa Dar es Salaam imepata neema kubwa chini ya Rais Samia kupitia ujenzi wa barabara ya njia nane kutoka Ubungo hadi Kimara kwa gharama ya shilingi bilioni 80, pamoja na flyovers katika maeneo ya Morocco na Mwenge ambazo zipo katika hatua za mwisho kukamilika. “Lengo ni kulifanya Dar es Salaam kuwa jiji la kimataifa linaloendana na kasi ya ukuaji wa Afrika Mashariki,” alihitimisha.




