Mhandisi Mshauri, Moon Dong Ryeol, anayesimamia barabara ya Itoni- Ludewa- Manda sehemu ya Lusitu- Mawengi (Km 50) inayojengwa kwa kiwango cha zege akifafanua jambo kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, anayeshughulikia Sekta ya Ujenzi, Mbunifu Majengo, Elius Mwakalinga (Kushoto), wakati akikagua barabara hiyo mkoani Njombe.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, anayeshughulikia Sekta ya Ujenzi, Mbunifu Majengo, Elius Mwakalinga, akitoa maagizo kwa Mhandisi Mshauri, Moon Dong Ryeol, anayesimamia barabara ya Itoni- Ludewa- Manda sehemu ya Lusitu- Mawengi (Km 50) inayojengwa kwa kiwango cha zege wakati akikagua barabara hiyo mkoani Njombe.
Mhandisi Mshauri, Moon Dong Ryeol, anayesimamia barabara ya Itoni- Ludewa- Manda sehemu ya Lusitu- Mawengi (Km 50) inayojengwa kwa kiwango cha zege akimuonesha Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, anayeshughulikia Sekta ya Ujenzi, Mbunifu Majengo, Elius Mwakalinga (Wa Kwanza Kushoto mbele), maungio ya zege yaliyopo katika barabara hiyo, mkoani Njombe.
Muonekano wa barabara ya Itoni- Ludewa- Manda sehemu ya Lusitu- Mawengi (Km 50) inayojengwa kwa kiwango cha zege, mkoani Njombe.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, anayeshughulikia Sekta ya Ujenzi, Mbunifu Majengo, Elius Mwakalinga, akitoa maelekezo kwa Mhandisi Mshauri kutoka SMEC International (katikati) anayesimamia barabara ya Mbinga – Mbamba Bay (Km 66) kwa kiwango cha lami. Barabara hiyo imefika asilimia 49.6.
PICHA NA WUUM
……………………………………………………………………………………………….
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, anayeshughulikia Sekta ya Ujenzi, Mbunifu Majengo, Elius Mwakalinga, amemtaka Mhandisi Mshauri anayesimamia barabara ya Itoni- Ludewa- Manda sehemu ya Lusitu- Mawengi (Km 50), inayojengwa kwa kiwango cha zege kujipanga upya kutokana na kutoridhishwa na kasi ya utendeji kazi ya mkandarasi wa mradi huo.
Akizungumza wakati akikagua mradi huo mkoani Njombe, Mwakalinga amemuagiza Mhandisi Mshauri huyo kuhakikisha anawasilisha taarifa zote na muhtasari wa vikao wanavyokaa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), ofisini kwake, ili aone kama anahifadhi taarifa hizo na anatekeleza yatokanayo na vikao hivyo.
“Sijafurahishwa na utendaji kazi wa Mkandarasi, nimewaagiza waniletee taarifa zao zote pamoja na muhtasari wa vikao vyote wanavyokaa wakiwa na TANROADS ili nione kama anatekeleza maagizo anayopewa, na kama hatekelezi ni kwa nini yupo mpaka sasa hivi”, amesema Mwakalinga.
Mwakalinga, amefafanua kuwa Mkandarasi huyo hajawajibika kama inavyotakiwa kwani kuna baadhi ya maeneo alitakiwa awe amefanya kazi zaidi, licha ya kuelezea kuwa na changamoto ya hali ya hewa, uhaba wa rasilimali watu na vifaa, jambo ambalo akijipanga vyema linaweza kutatulika.
Mwakalinga, ameongeza kuwa lengo la kutaka mradi huo kuharakishwa ni kutokana na umuhimu wa barabara hiyo katika kukuza uchumi kwani ni kiungo cha usafiri na usafirishaji wa watu na mizigo kati ya mkoa wa Njombe na Ruvuma.
Kwa upande wake, Mhandisi Mshauri wa mradi huo, Moon Dong Ryeol, amemhakikishia Katibu Mkuu huyo kuwa ataleta wataalamu wengine wa kusaidia kuongeza nguvu ya usimamizi pamoja na kuongeza kasi ya ujenzi na muda wa kufanya kazi.
Aidha, Ryeol, ameahidi kununua mtambo wa pili wa kuzalisha zege pamoja na mashine ya kisasa ya kuweka tabaka la zege ili kwa pamoja visaidie katika ufanisi wa mradi huo.
Katika hatua nyingine, Mwakalinga amekagua barabara ya Mbinga – Mbamba Bay yenye urefu kilometa 66 ambapo ameridhishwa na utendaji kazi wa Mkandarasi anayejenga mradi huo.
Mwakalinga, amesema kuwa mradi huo sio tu kwamba unatekelezwa kwa haraka, bali pia unajengwa kwa ubora kwani mkandarasi amejipanga na kuzingatia misingi ya kitaalamu ya ujenzi wa barabara.
Sambamba na hilo, Mwakalinga, wakati akikagua barabara hiyo, wilayani Nyasa mkoani Ruvuma, amefafanua kuwa mpaka sasa mradi unaendelea vizuri kwani mkandarasi yupo ndani ya mkataba na anaamini kwa utaratibu anaoenda nao, mkandarasi huyo anaweza kumaliza kazi hiyo kwa wakati.
“Nimekagua mwanzo hadi nwisho wa mradi, kwa kweli kazi imefanyika haswa tena yenye ubora, nampongeza mkandarasi huyu kwa kufanya kazi kwa juhudi kubwa, naomba endelea kukamilisha kipande kilichobakia”, amesema Mwakalinga.
Katika hatua nyingine Mwakalinga, amekagua daraja la Mto Ruhuhu ambapo amesema kuwa kwa sasa ujenzi wa daraja hilo umesimama kutokana na mto kufurika maji na wataalamu kushindwa kuendelea mpaka maji yatakapopungua.
Ukaguzi huu ni mwendelezo wa ziara ya Katibu Mkuu Mwakalinga katika mikoa mbalimbali nchini ili kukagua miradi inayotekelezwa na Sekta ya Ujenzi.