Na Neema Mtuka – Sumbawanga
RUKWA: Mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema akipata ridhaa ya kuendelea kuongoza nchi, atahakikisha wanatoa maji kutoka Ziwa Tanganyika ili kuanzisha gridi ya taifa ya maji.
Dkt. Samia ameyasema hayo leo Oktoba 19, 2025, wakati wa mkutano wa kampeni uliofanyika katika uwanja wa Shule ya Sekondari Kizwite, Manispaa ya Sumbawanga, mkoani Rukwa.
Amesema mradi huo utakapo kamilika utasaidia kuondoa changamoto ya ukosefu wa maji safi na salama na kumtua mama ndoo kichwani.
“Mradi huu wa maji utawaondolea wananchi adha ya kutembea umbali mrefu kufuata maji, na utaleta mahusiano mazuri katika familia,” amesema Dkt. Samia.
Akiwa katika mkutano wa kampeni, Dkt. Samia amewaomba wananchi wa Rukwa kumchagua kwa nafasi ya urais na kuwaombea wabunge wa majimbo matano ya mkoa wa Rukwa pamoja na madiwani wa kata 97 waliojitoa kugombea nafasi hizo.
Kwa upande wake, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, amesema mkoa wa Rukwa una jumla ya vijiji 347 ambavyo vimefikiwa na huduma ya maji safi na salama kwa zaidi ya asilimia 84.
Amesema serikali itaendelea kuvifikia vijiji vyote ambavyo havina huduma hiyo ya maji safi na salama.
“Serikali itaendelea kuhakikisha inawafikia wananchi wote ili wapate maji safi na salama kulingana na bajeti itakavyokuwa inatoka,” amesema Aweso.
Naye Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, amesema serikali itajenga maghala ya kuhifadhia mahindi yenye uwezo wa tani laki nne mkoani Rukwa.
Bashe amesema maghala hayo yanajengwa kutokana na uzalishaji mkubwa wa zao la mahindi katika mkoa wa Rukwa.
Pia Waziri Bashe amesema shamba lililopo katika Kijiji cha Nkundi, Wilaya ya Nkasi, linarudishwa mikononi mwa serikali.
Aliyekuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Ezekiel Wenje, amesema kuna kila sababu ya kukichagua Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutokana na kazi kubwa ya kiongozi bora, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Amesema miradi ya maendeleo ndiyo inayowaunganisha Watanzania wote, na amewataka Watanzania kuungana na kumchagua Dkt. Samia Suluhu Hassan ili aendeleze pale alipoishia.
“Kwa dhamira yangu naamini nimechagua njia salama. Nilipokuwa kule nilipotea. Nasisitiza kuwa kupiga kura ni haki ya msingi ya kikatiba, hivyo kila Mtanzania ana haki ya kupiga kura,” amesema Wenje.
Aidha, Mgombea Ubunge wa Jimbo la Sumbawanga Mjini, Aeshi Halfan Hilaly, amesema Dkt. Samia ameweza kuimarisha uchumi tangu alivyoingia madarakani.