NA JOHN BUKUKU- SUNBAWANGA
Chifu Kapere Said Kapere kutoka Wilaya ya Nkasi, akizungumza, Mjini Sumbawanga amesema kuwa ujio wa Mgombea Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, ni tukio adhimu na muhimu kwa wananchi wa Mkoa wa Rukwa.
Ameyasema hayo katika muendelezo wa kampeni za Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan, uliofanyika Uwanja wa Kizwite, Mjini Sumbawanga, mkoani Rukwa, Oktoba 19, 2025.
Amesema ujio huo ni fursa kwa wananchi kueleza changamoto zao, huku akibainisha kuwa kwa kiasi kikubwa changamoto hizo zimepungua kutokana na utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2020–2025 chini ya uongozi wa Mama Samia.
Aidha, ameeleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kufungua uchumi wa Mkoa wa Rukwa na taifa kwa ujumla kupitia miradi mikubwa ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa barabara kutoka Matai, ambayo itawekwa lami na kuchochea uchumi wa Ziwa Tanganyika unaounganisha Tanzania, Zambia na Kongo.
Chifu Kapere amesema licha ya changamoto za kipindi cha ugonjwa wa COVID-19, Dkt. Samia aliweza kusimama imara na kuimarisha uchumi wa nchi, hatua iliyosaidia kuongeza kipato cha wananchi na kuboresha huduma za kijamii kama hospitali, shule na vyuo vya elimu ya juu.
Ameongeza kuwa ndani ya mkoa huo, vyuo vya VETA na Ualimu vimeanzishwa katika wilaya zote tatu, huku akiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kujenga chuo kikuu mjini Sumbawanga ili kutoa fursa zaidi za elimu kwa vijana wa Rukwa.
Amesema kuwa Dkt. Samia ni kiongozi shupavu na mtetezi wa wanawake, akiwakumbusha wananchi kuwa mwaka 2016 aliteuliwa na Umoja wa Mataifa (UN) kuwa mjumbe wa uwezeshaji wa wanawake kusini mwa Jangwa la Sahara — hatua inayoonyesha dhamira yake ya kuwawezesha wanawake kiuchumi na kiutawala.
Aidha, amehimiza umuhimu wa kudumisha amani na utulivu katika kipindi cha uchaguzi, akiwataka Watanzania kujitokeza kwa wingi kupiga kura kwa amani na kuepuka vurugu.
Chifu Kapere amewataka vijana kuepuka kushiriki vitendo vya fujo, badala yake kuelekeza nguvu zao katika kujenga maisha kupitia kazi, bidii na uadilifu. Amesisitiza kuwa nchi ipo katika hali ya furaha na utulivu mkubwa unaopaswa kulindwa na kila mmoja.
Aidha, amebainisha kuwa Serikali imeendelea kutoa ajira mbalimbali, ikiwemo za ualimu, hivyo amewataka vijana kujitokeza kuomba nafasi hizo ili wachangie katika maendeleo ya taifa.
Amehitimisha kwa kusisitiza kuwa hakuna mafanikio bila kufanya kazi, akiwahimiza vijana kutumia fursa zinazotolewa na Serikali kwa manufaa yao na jamii kwa ujumla.