Kutoka Mahakama ya Wilaya ya Missenyi
Leo tarehe 17 Oktoba 2025, Mahakama ya Wilaya ya Missenyi chini ya Hakimu Mfawidhi, Mh. Yohana Muyombo, imemhukumu mfanyabiashara Martine Muyobya Tabura kwenda jela miaka mitatu baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kushiriki vitendo vya rushwa kinyume na kifungu cha 15(1)(a) na (2) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Sura ya 329, Marejeo ya Mwaka 2023.
Imeelezwa mahakamani kuwa kati ya tarehe 11 hadi 25 Julai 2025, mshtakiwa akiwa mfanyabiashara, aliingiza nchini kutoka Uganda vifaa vya muziki vyenye thamani ya Sh. 9,285,714/= kwa njia za magendo bila kulipa kodi ya Serikali, na hivyo kujipatia manufaa yasiyo halali ya Sh. 3,958,118/=, ambayo ndiyo kodi stahiki ya Serikali.
Baada ya usikilizaji wa shauri hilo, Mahakama imemkuta mshtakiwa na hatia na kumpa adhabu ya kifungo cha miaka mitatu jela bila faini.
Shauri hilo limeendeshwa na waendesha mashtaka wa TAKUKURU, Bw. Sospeter Joseph na Bw. William Musso.