Na Mwandishi Wetu – Holili, Kilimanjaro
Mnamo Oktoba 15, 2025, katika Mahakama ya Wilaya ya Rombo mbele ya Hakimu Mkuu Mwandamizi, Mhe. Innocent Nyella, kesi ya jinai namba 9081/2025 ilihusisha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania dhidi ya Hemrod Elias Ngunga, fundi bomba wa ROMBOWSSA.
Ngunga alishtakiwa kwa kosa la kushawishi, kuomba na kupokea hongo kinyume na vifungu vya 15(1)(a)(b)(2) vya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Sura ya 329, Marejeo ya Mwaka 2022.
Mawakili wa Serikali, Bi. Furahini Kibanga na Bw. Anold Mafwele, walieleza kuwa mshtakiwa alipokea hongo ya Sh. 20,000/= kutoka kwa mteja ili kumsaidia kurejeshewa mita zake za maji zilizokuwa zimeibiwa katika eneo la Holili.
Mahakama ilimkuta mshtakiwa na hatia na kumuamuru kulipa faini ya Sh. 300,000/= au kutumikia kifungo cha miaka mitatu jela. Kwa kuwa ameshindwa kulipa faini, amepelekwa rumande kutumikia adhabu hiyo.