*Amesisitiza kuchagua viongozi sahihi
*Kura za urais apewe Dk. Samia wa CCM
Na Mwandishi Wetu, Bariadi
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira amesema nchi ipo salama, wananchi wakumbushwe na kuhamasishawa kuwapigia kura wagombea wenye sifa ambapo kwa upande wa urais ni Dk. Samia Suluhu Hassan anayetokana na CCM.
Amesema zipo propaganda chafu katika mitandao ya kijamii lakini yanayooelezwa ni upotoshaji, hayana ukweli kwa lengo la kupotosha umma.
Makamu Mwenyekiti Wasira alieleza hayo alipokuwa akizungumza na viongozi wa CCM wilayani Bariadi Mkoa wa Simiyu, leo Oktoba 18, 2025.
“Wako watu katika nchi yetu ambao wanakerwa na amani na wanashirikiana na watu wa nje kutaka kuwavuruga.
“Siku hizi kuna mitandao ya kijamii inapeleka habari za uongo, kutisha na kuwafanya watu wafikiri kuna shida, mimi, nakuja kuwaambia nchi ipo salama kabisa, nchi yetu iko salama na zimebaki siku 10 twende tukapige kura,” alisema.
Alisisitiza viongozi wa Chama katika ngazi mbalimbali kuwahamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi mapema asubuhi siku ya kupiga kura watimize haki yao ya msingi kuchagua viongozi wanaofaa.
“Nimekuja kuwaambia nendeni muwaambie Watanzania wenzetu tangu shina wajitokeze kwa wingi waende wapige kura kwa sababu mamlaka ya nchi yapo mikononi mwao, na ndio wakati wao wa kukabidhi madaraka haya kwa watu wanaowaamini,” alielekeza.
Wasira alifafanua kuwa, wananchi wanapaswa kuchagua viongozi wenye weledi, uadilifu na uaminifu katika kuwatumikia Watanzania.