Afisa
miradi kutoka TEA Bi. Atugonza David akikagua maabara ya Sayansi Shule ya Sekondari
Itumba ambayo imekarabatiwa na kumaliziwa ujenzi na TEA kwa kushirikiana na
UNICEF, kupitia ufadhili wa Serikali ya Canada.
:::::::::::
Na Mwandishi Wetu, Songwe
Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) kwa
kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) wameendelea
kufanya mapinduzi makubwa katika kuinua ubora wa elimu nchini, hususan katika
masomo ya sayansi. Hatua hii ni sehemu ya utekelezaji wa makubaliano maalum
yaliyosainiwa kati ya pande hizo mbili, yakilenga kuboresha miundombinu ya
elimu kwa kujenga na kukarabati maabara za sayansi katika shule mbalimbali za
mikoa ya Songwe, Kigoma na Tabora.
Halmashauri ya Wilaya ya Ileje mkoani
Songwe ni moja kati ya wilaya zilizonufaika na mapinduzi haya ambapo shule
mbili zimenufaika na umaliziaji wa ujenzi wa maabara nne za Sayansi. Umaliziaji
ujenzi na ukarabati wa maabara hizo unafanyika kwa ufadhili wa Serikali ya
Canada, ambapo takribani shilingi milioni 132 zimetumika.
Akizungumza wakati wa ukaguzi wa miradi
hiyo, Afisa Miradi kutoka TEA, Bi Atugonza David, alisema shule zilizonufaika
ni Shule ya Sekondari Itumba, iliyopokea ruzuku ya shilingi milioni 78.3
kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa vyumba viwili vya maabara, na Shule ya
Sekondari Bupigu, iliyopokea ruzuku ya shilingi milioni 54 kwa ajili ya
kumalizia ujenzi wa maabara mbili za Kemia na Fizikia.
Mkuu wa Shule ya Sekondari Itumba, Mwl.
Didiye Paul, alieleza kuwa ufadhili huo umekuwa wa neema kubwa kwa shule yake
ambayo awali haikuwa na maabara hata moja.
“Awali wanafunzi wetu walikuwa
wakifanyia mazoezi ya sayansi darasani, jambo lililokuwa likipunguza ufanisi wa
ujifunzaji. Kukamilika kwa maabara hizi kumetoa hamasa kubwa na idadi ya
wanafunzi wanaojisajili kusoma masomo ya sayansi imeongezeka kwa asilimia 75
kutokana na mazingira kuwa rafiki na ya kuvutia,” alisema Mwl. Paul.
Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya
Sekondari Bupigu, Mwl. Shuhudia Mbembela alisema, kilio cha kukosekana kwa
maabara ni cha siku nyingi kwa walimu na wanafunzi shuleni hapo hivyo ufadhili
walioupata umekuwa mkombozi wao.
“Hadi sasa tumeshakamilisha ukarabati wa
maabara moja na nyingine ukarabati unaendelea umefikia asilimia 95,” alisema
Mwl. Mbembela.
Mwl. Mbembela aliongeza kuwa kukamilika
kwa maabara hizo ni kutimia kwa ndoto ya muda mrefu ya shule hiyo, kwani hapo
awali wanafunzi na walimu walikuwa wakifanya mafunzo kwa vitendo katika
mazingira magumu na yasiyo salama.
“Sasa tunaamini ufaulu katika masomo ya
sayansi utaongezeka kwa kiwango kikubwa,” alisisitiza.
Kwa ujumla, Mamlaka ya Elimu Tanzania
(TEA) kwa kushirikiana na UNICEF inaendelea kutekeleza miradi
mbalimbali yenye thamani ya takribani shilingi bilioni 3 katika mikoa
ya Songwe, Kigoma na Tabora. Miradi hiyo inalenga kuinua ubora wa elimu,
kuboresha mazingira ya kujifunzia, na kupanua fursa za elimu bora na salama kwa
kila mtoto wa Kitanzania.
MMuonekano
wa ndani wa maabara ya sayansi Shule ya Sekondari Itumba zilizokamilishwa na
TEA kwa kushirikiana na UNICEF, kupitia ufadhili wa Serikali ya Canada.
Muonekano
wwa ndani wa maabara ya sayansi Shule ya Sekondari Itumba zilizokamilishwa na
TEA kwa kushirikiana na UNICEF, kupitia ufadhili wa Serikali ya Canada.
wa Shule ya Sekondari Itumba Mw. Didiye Paul (katikati) akiwa pamoja na Afisa
miradi kutoka TEA Bi. Atugonza David wakikagua maabara mbili za sayansi shuleni
hapo zilizokamilishwa na TEA kwa kushirikiana na UNICEF, kupitia ufadhili wa
Serikali ya Canada.
wa Shule ya Sekondari Bupigu Mwl. Shuhudia Mbembela akitoa maelezo kwa Afisa
miradi kutoka TEA Bi. Atugonza David, wakati wa ukaguzi wa umaliziaji ujenzi wa
maabara mbili za Sayansi shuleni hapo.
Mkuu
wa Shule ya Sekondari Bupigu Mw. Shuhudia Mbembela akiwa pamoja na Afisa miradi
kutoka TEA Bi. Atugonza David wakikagua maabara mbili za sayansi shuleni hapo
zilizokamilishwa na TEA kwa kushirikiana na UNICEF, kupitia ufadhili wa
Serikali ya Canada.