Mgombea ubunge Viti Maalumu mkoa wa Arusha , Marirta Gido akizungumza na madereva bajaji pamoja na pikipiki jijini Arusha leo
……..
Mgombea ubunge Viti Maalumu mkoa wa Arusha , Marirta Gido amewataka vijana kuhakikisha Oktoba 29 wanajitokeza kwa wingi kupiga kura kwa maslahi ya maendeleo ya wananchi na ustawi wa Arusha mpya.
Ameyasema hayo leo jijini Arusha wakati akizungumza katika mkutano uliowakutanisha madereva wa bodaboda na bajaji zaidi ya 100.
Aidha amesema kuwa , ni wajibu wa vijana hao kuhakikisha wanajitokeza kwa wingi kwenda kupiga kura kwani ni haki yao ya msingi kufanya hivyo.
Ameongeza kuwa, vijana hao pia wana wajibu mkubwa wa kuhamasisha vijana wenzao kujua umuhimu wa kupiga kura na kuwachagua viongozi watakaokuwa na maslahi na nchi yao katika kuleta maendeleo na kuondokana na changamoto mbalimbali.
“Tunashuhudia kazi kubwa iliyofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan katika Mkoa wa Arusha, ikiwemo kutoa mkopo wa shilingi bilioni 200 kwa ajili ya kuwainua kiuchumi vijana wa Arusha Mjini na kila mmoja ameona jinsi ambavyo mkopo huo umeleta mafanikio makubwa kwa vijana pamoja ja kuwainua kiuchumi. “amesema.
Aidha, amesema mikopo hiyo ni sehemu ya uwezeshaji wa kiuchumi kwa vijana, hivyo ushiriki wao katika maamuzi ya kisiasa ni nyenzo muhimu ya kuendeleza juhudi za serikali.
Kwa upande wao, baadhi ya madereva wa bodaboda na bajaji wameeleza kuwa wana shauku kubwa ya kuona Arusha inaendelea kuwa eneo salama lenye fursa nzuri za utafutaji kupitia biashara ya usafirishaji.