NA JOHN BUKUKU- KAGERA
Mgombea wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema kuwa serikali imejipanga kujenga uwanja mkubwa wa kimataifa wa ndege katika Wilaya ya Misenyi, mkoani Kagera, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuufungua mkoa huo kiuchumi na kiutalii.
Akizungumza na wananchi katika viwanja vya Bashungwa, Kayanga mkoani humo, Oktoba 15, 2025, Dkt. Samia amesema kuwa ujenzi wa uwanja huo ni utekelezaji wa Ilani mpya ya CCM inayolenga kuimarisha sekta za uzalishaji na miundombinu ya usafiri na usafirishaji.
Amesema Mkoa wa Kagera kwa sasa una kiwanja kimoja kidogo cha Bukoba, hivyo kujengwa kwa kiwanja kingine kikubwa katika Wilaya ya Misenyi kutaupa mkoa huo fursa kubwa ya kibiashara na kiutalii.
“Ilani yetu inatuelekeza kujenga kiwanja cha pili ndani ya mkoa huu, na kiwanja hicho kitajengwa Wilaya ya Misenyi. Kitakuwa ni kiwanja kikubwa cha kimataifa kitakachowezesha ndege kubwa kutua na kuondoka, hivyo kuufungua mkoa huu kibiashara na kiutalii,” amesema Dkt. Samia.
Dkt. Samia amebainisha kuwa ujenzi wa uwanja huo utakwenda sambamba na miradi mingine ya barabara na bandari inayotekelezwa katika Mkoa wa Kagera, ikiwemo bandari za Kemondo na Bukoba, ili kuboresha usafiri na usafirishaji wa bidhaa na watu.
Aidha, amesema kuwa serikali inaendelea kuimarisha sekta nyingine muhimu kama kilimo, viwanda, elimu, afya, maji na nishati, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kukuza uchumi wa wananchi na taifa kwa ujumla.
“Maendeleo ni safari na hatua. Tunakwenda hatua kwa hatua, tukijenga miundombinu ya msingi itakayowawezesha wananchi kushiriki moja kwa moja kwenye uchumi wa taifa,” amesema Dkt. Samia.
Aidha, Dkt. Samia amebainisha kuwa uwanja huo wa ndege wa kimataifa utasaidia kuvutia wawekezaji na watalii kutoka ndani na nje ya nchi, jambo litakalosaidia kuongeza mapato na ajira kwa wakazi wa Mkoa wa Kagera na maeneo jirani.