Rasi wa Chuo Kishiriki cha Elimu Mkwawa Profesa Method Semiono akizungumza na wanahabari.
………..
NA DENIS MLOWE IRINGA
Chuo Kishiriki cha Elimu Mkwawa (MUCE), kikiwa chini ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), kimepongeza juhudi kubwa za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa katika sekta ya elimu, kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (Higher Education for Economic Transformation – HEET Project).
Katika taarifa iliyotolewa Rasi wa Chuo Kishiriki cha Mkwawa, Profesa Method Semiono ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya kumbukizi ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere amesema kuwa mradi huo ni matokeo ya dhamira ya Serikali ya kuendeleza elimu ya juu ili kuchochea mageuzi ya kiuchumi nchini.
Alisema kuwa mradi wa wa HEET ambao serikali ya Rais Samia umekuwa na Uwekezaji wa Kimkakati katika elimu nchini ikiwa unatekelezwa kwa miaka mitano (2021/2022–2025/2026) unafadhiliwa na Benki ya Dunia na unalenga kuboresha ubora wa elimu ya juu nchini.
Profesa Semioni alisema kuwa kupitia mradi huo MUCE imetengewa kiasi cha Dola za Kimarekani milioni 8 (sawa na Shilingi Bilioni 18.6 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimkakati.
Alisema kuwa Fedha hizo zinatumika katika maeneo sita muhimu: ikiwemo Uboreshaji wa mitaala na mbinu za ufundishaji, Ujenzi wa miundombinu ya kisasa , Kuendeleza rasilimali watu kuimarisha elimu jumuishi na usawa wa kijinsia na Kuboresha matumizi ya TEHAMA na majukwaa ya kidijitali na Kuimarisha uhusiano kati ya vyuo na sekta binafsi.
Profesa Semiono alisema kuwa uboreshaji wa Mitaala na Ubunifu katika Elimu kupitia HEET, MUCE imefanya mapitio ya mitaala mitano ya zamani na kuanzisha mitaala mipya 30 inayolenga kuongeza ujuzi unaokidhi mahitaji ya soko la ajira.
Aidha, Chuo kimeanzisha programu saba za Umahiri (Masters) na mbili za Uzamivu (PhD), na hivyo kufikisha jumla ya programu 14 za uzamivu kutoka tano (5) za awali hii katika awamu ya sita chini ya Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Hatua hii imeongeza fursa za udahili, ambapo idadi ya wanafunzi inatarajiwa kufikia 10,000. Mitaala mipya inajikita katika kukuza ubunifu, elimu ya fedha, akili mnemba, na ujuzi wa msingi (soft skills) unaowezesha wahitimu kujiajiri au kuajirika.
Vilevile Ujenzi wa Miundombinu ya Kisasa katika kuboresha mazingira ya kujifunzia, MUCE imetengewa zaidi ya Shilingi Bilioni 15.29 kwa ajili ya ujenzi wa majengo manne makubwa ambayo ni jengo la Hosteli za Wanafunzi lenye ghorofa mbili na vyumba vya kusomea, jengo la Maabara ya Fizikia lenye kituo cha hali ya hewa jengo la Midia Anuwai na Elimu Maalumu lenye miundombinu ya wanafunzi wenye ulemavu na Jengo la Sayansi litakalokuwa kituo kikuu cha mafunzo na tafiti za sayansi lenye maabara za kisasa.
Aidha alisema kuwa Serikali imetoa zaidi ya Shilingi Bilioni 15 nyingine kwa ajili ya miradi mingine ya maendeleo, na kufanya jumla ya fedha zilizotolewa kwa miundombinu ya MUCE kufikia zaidi ya Shilingi Bilioni 30.
Miundombinu hiyo itasaidia kuongeza udahili wa wanafunzi kwa zaidi ya elfu nne na kupunguza changamoto ya upungufu wa hosteli kwa wanafunzi wanaoishi nje ya kampasi.
Mageuzi ya TEHAMA na Ufundishaji wa Kidijitali.
Katika nyanja ya TEHAMA, MUCE inatekeleza ukarabati mkubwa wa mifumo ya teknolojia ya mawasiliano na kutandaza nyaya za fibre kwa ajili ya mtandao wa intaneti wa kasi. Ujazo wa intaneti umeongezwa, na majukwaa ya ufundishaji kwa njia ya mtandao yameanzishwa.
Kwa hatua hii, wanafunzi kutoka maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi wanaweza kupata elimu ya juu kupitia mfumo wa kidijitali, bila kulazimika kufika chuoni.
Alimalizia kusema kuwa kupitia mradi wa HEET, Serikali ya Awamu ya Sita imefanikisha mageuzi makubwa katika elimu ya juu nchini uwekezaji huu katika MUCE ni kielelezo cha dhamira ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuendeleza elimu bora, jumuishi na yenye tija kwa maendeleo ya taifa.
Alitoa wito kwa jamii kujitokeza kwa wingi kupiga kura Oktoba 29 kwa Dkt Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya miradi mbalimbali amhayo imeleta na italeta tija kwa nchi.
Kwa upande wake Rais wa Serikali ya wanafunzi wa Chuo Kishiriki cha Elimu Mkwawa, Musa Mgema alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kufanikisha miradi ya makazi wa wanafunzi katika chuo hicho.
Alisema kuwa ujenzi wa hostell kwa ajili ya wanafunzi itasaidia usalama kwa wanafunzi na kuwaweka sehelmu salama ambapo awali wengi walikuwa wanaishi nje ya chuo na kuongeza kuwa ujenzi huo utasaidia kupata mazingira bora ya kusomea.