Na: Dkt. Reubeni Lumbagala, Tanga
Oktoba 14, 1999, ilikuwa ni siku ya simanzi kubwa nchini kwetu Tanzania baada ya kutangazwa kifo cha Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Leo, Jumanne ya Oktoba 14, 2025, imetimia miaka 26 tangu kutokea kifo chake.
Kimsingi, Hayati Mwalimu Nyerere alikuwa ni hazina kubwa kwa Taifa letu, hazina ambayo hakuna maneno wala kitabu kitakachotosha kuelezea maisha yake. Moja ya dhamira ya Mwalimu Nyerere tangu akiwa Rais na hata baada ya kustaafu, alitamani kuona Watanzania wakiishi maisha ya ustawi, mbali na umaskini.
Aliweka mkazo mkubwa kwa serikali kufanya kila liwezekanalo, lililo katika uwezo wake kuhakikisha tatizo la umaskini linatatuliwa. Aliweka mkazo katika ukusanyaji kodi ili fedha hizo zitumike katika kutekeleza mipango mbalimbali ya serikali kwa ajili ya ustawi wa wananchi.
Alitaka kila Mtanzania mwenye sifa za kulipa kodi alipe. Hakutaka serikali ikusanye kodi kwa uonevu wala mabavu. Alitaka raia wote wa ngazi za chini, kati na juu waunganishe nguvu zao kwa pamoja katika ujenzi wa Taifa lao kupitia ukusanyaji kodi. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inawajibika moja kwa moja kukusanya kodi kutoka kwa wananchi wake kwa kushirikiana na mamlaka za serikali za mitaa katika Halmashauri zetu.
Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda, Oktoba 2, 2025, alitoa taarifa ya makusanyo ya kodi kwa kipindi cha robo ya mwaka ya mwaka wa fedha 2025/2026 (Julai hadi Septemba 2025). “TRA imefanikiwa kukusanya kiasi cha Shilingi Trilioni 8.97 sawa na ufanisi wa asilimia 106.3 ya lengo la kukusanya Shilingi Trilioni 8.44. Makusanyo hayo ni sawa na ukuaji wa asilimia 15.1 ikilinganishwa na kiasi cha Shilingi Trilioni 7.79 kilichokusanywa katika kipindi kama hicho cha mwaka wa fedha 2024/2025,” ilieleza taarifa hiyo ya Kamishna Mkuu wa TRA.
Kwa hakika kazi kubwa imefanywa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia katika kuhakikisha kodi zinakusanywa kikamilifu ili zitumike katika kuboresha hali za maisha ya Watanzania katika sekta mbalimbali kama vile maji, kilimo, afya, elimu, umeme, barabara, viwanda, biashara, masoko, vituo vya mabasi, uwezeshaji wananchi kiuchumi, kutaja kwa uchache. Aidha, taarifa hiyo ya Kamishna Mkuu wa TRA pia inaonyesha kwa mwezi Septemba, 2025 pekee, TRA imefanikiwa kukusanya Shilingi Trilioni 3.47.
Mafanikio katika ukusanyaji kodi yanatoa uhakika wa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo inagusa maisha ya wananchi moja kwa moja hasa katika kuwaletea maendeleo na kupunguza umaskini unaowakabili. Hayati Mwalimu Nyerere aliwahi kusema “Kila Mtanzania anapaswa kuelewa kwamba maendeleo hayawezi kupatikana kwa kutegemea misaada, ni lazima tulipe kodi.”
Hivyo basi, tunapoadhimisha miaka 26 ya kifo cha Hayati Mwalimu Nyerere, tuna kila sababu ya kujivunia uongozi wa Rais Dkt. Samia ambao umesimama imara katika ukusanyaji kodi bila kutumia mabavu wala uonevu, huku mwamko wa wananchi kulipa kodi ukiongezeka kutokana na uwepo wa mazingira mazuri ya ufanyaji biashara na namna wananchi wanavyoona kodi zao zinavyorudi kwao kwa njia ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Mwandishi wa makala hii ni Mwalimu wa Shule ya Sekondari Funguni iliyopo wilayani Pangani mkoani Tanga.
Maoni: 0620 800 462.