…………..
NA DENIS MLOWE, IRINGA
TIMU ya Soka ya Young Stars imefanikiwa kuibuka mabingwa wa Iringa Super Cup kwa kuwafunga magoli 3 – 2 imu ya soka ya Kipigwe Fc katika mtanange uliopigwa kwenye uwanja shule ya msingi Mlandege.
Katika mchezo huo uliohudhuriwa na maelfu ya mashabiki wakishuhudia mchezo uliowakutanisha vijana wadogo wenye uwezo mkubwa wa Young Stars chini ya mwalimu wa mpira Saidi Chitalula wakikutana na wachezaji wakubwa na wenye uzoefu wa Kipigwe fc.
Katika mchezo huo mgeni rasmi alikuwa aliyekuwa mbunge wa Iringa Mjini Jesca Msambatavangu ambapo alikabidhi zawadi ya Ng’ombe kwa nahodha wa Young Stars.
Akizungumza kabla ya kukabidhi zawadi kwa washindi, Msambatavangu aliwapongeza waratibu wa mashindano hayo na wadhamini kampuni ya mawasilano ya Yas kwa kudhamini wa mashindano hayo ambayo yameibua vipaji kwa wachezaji vijana katika mkoa wa Iringa.
Msambatavangu alisema kuwepo kwa mashindano mbalimbali na ya mara kwa ni moja ya njia bora ya kuibua vipaji kwa vijana na kuzalisha ajira.
Alisema kuwa mkoa wa Iringa unahitaji wadau mbalimbali kujitokeza kudhamini mashindano yanaandaliwa na chama cha soka au wadau wenyewe ikiwa lengo kubwa ni kukuza soka la mkoa.
“Hivyo basi niwapongeze sana wadau na wadhamini wa mashindano ndani ya mkoa wa Iringa kwani bandikabandua itasaidia kwa kiasi kikubwa kuibua vipaji vya vijana na kuongeza ajira.” Alisema.
Msambatavangu vilevile aliwagusia wanamichezo kujitokeza tarehe Oktoba 29 kupiga kura na kutohofia maneno ambayo yanasambazwa na wachache kwamba kutakuwa na maandamano.
Katika mashindano hayo bingwa aliondoka na Ng’ombe, mshindi wa pili timu ya Kipigwe waliondoka na laki 3 wakati mshindi wa tatu timu ya Isakalilo fc waliondoka na sh laki mbili.