NA DENIS MLOWE, IRINGA
ALIYEKUWA Meya wa Manispaa ya Iringa, Ibrahim Ngwada amewataka wananchi wa kata ya Ilala kuachana na kuyapuuza maneno yanayosambazwa na baadhi ya watu wasiopenda amani nchini.
Akizungumza wakati kampeni za mgombea ubunge jimbo la Iringa Mjini Fadhili Ngajilo, Ngwada ambaye anagombea udiwani kata ya Mshindo alisema kuwa kumekuwa na maneno kwa baadhi ya watu katika mitandao ya kijamii kwamba kutakuwa na maandamano na kutokea vurugu siku ya Oktoba 29 wawapuuze na wakaandamane katika familia zao.
Alisema kuwa uchaguzi utakuwepo kama ambavyo katiba inasema hivyo watu wasiwe na wasiwasi wajitokeze siku ya kupiga kura kwa kuwa serikali imejipanga vyema katika kulinda amani ya nchi.
Ngwada alisisitiza kuwa wananchi waelewe kwamba asitokee mtu yoyote akawatishia amani siku ya kupiga kura bali waakishe wanapiga kura za kutosha kwa mgombea urais Dk Samia Suluhu Hassan ili maendeleo yawafikie wengi zaidi.
Aliongeza kuwa wananchi wasiogope maneno kwamba watakinukisha waende wakafanye hayo kwenye familia zao ila kwa serikali hii hakuna wa kuwatisha kwa kuwa ni haki yenu kupiga kura kwa amani na utulivu.
“Asitokee mtu kuogopa kwani nchi yetu ni nchi ya usalama na wengi tumesikia kauli ya rais Samia kuhusu amani hivyo amani ipo na mjitokeze kwa wingi katika kupiga kura ” Alisema.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Iringa, Said Rubeya aliwataka kuendelea kupuuza na kuacha kuwanadani watu ambao wamekuwa wakitangaza uvunjifu wa amani kwani hawana la maana na hawawezi zuia chaguzi iliyoko kwenye katiba.
Alisema kuwa Hakuna kunuka wala kunukisha watanuka wenyewe hivyo wanachi wanachotakiwa kujitokeza kwa wingi na kukipa kura za kishindo chama cha Mapinduzi hususani wagombea wake wa urais, ubunge na udiwani katika jimbo la Iringa mjini.
Naye Mgombea ubunge wa jimbo la Iringa mjini Fadhili Ngajilo alisema kuwa atahakikisha changamoto zote katika kata ya Ilala kwa kushirikiana na diwani Godfrey Mlowe endapo watapewa kura watazishughulikia.
Alisema kuwa changamoto za miundo mbinu kama madaraja watahakikisha wanawaambia tarura wafanye kwa ajili ya kutumika ifanyike.
Akizungumzia changamoto ya jamii kama mikopo atahakikisha wanatoa elimu kwa wajasiriamali kuepuka mikopo ya kausha damu hivyo watahakikisha wananchi wanapata mikopo yenye riba nafuu na , kuongeza kuwa watahakikisha kilimo kinaongeza uzalishaji kwa kuwawezesha teknolojia za kisasa zaidi.
Ngajilo akielezea sekta ya afya katika kata ya Ilala atahakikisha hospital ya Frelimo itatoa huduma bora , ya uhakika na kuondoa kero kwa baadhi ya wahudumu wenye kutoa huduma mbovu.
Vile vile alisema kuwa sekta ya elimu wataisimamia kidete ili waweze kupata elimu bora na kwa kutumia wanavyuo watahakikisha wanalifanyia kazi suala kutoa elimu iliyobora jimboni Iringa.