Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Asha-Rose Migiro, leo amesisitiza umuhimu wa kazi, uzalishaji na uwajibikaji kama msingi wa kujenga uchumi imara wa taifa, wakati akihutubia wananchi wa Bukombe mkoani Geita.
Dkt. Migiro amesema kuwa Bukombe ni eneo lenye pumzi ya uzalishaji na watu wanaoamini katika kazi halisi, ambako kila jembe, kila mradi na kila mwananchi anashiriki kikamilifu katika safari ya kuijenga Tanzania yenye matokeo chanya.
Amesema miradi ya maendeleo inayoendelea katika sekta za nishati, maji, barabara na huduma za kijamii ni ushahidi tosha kwamba Chama Cha Mapinduzi hakiahidi tu — bali kinatenda kwa vitendo katika kuwaletea wananchi maendeleo.
Katika mkutano huo, Dkt. Migiro amempongeza Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Mashaka Biteko, ambaye pia ni mwana wa Bukombe, kwa mchango wake mkubwa katika kusukuma mbele ajenda ya maendeleo kupitia sekta ya nishati ya taifa.
Akiwahutubia maelfu ya wananchi waliofurika katika mkutano huo wa hadhara, Katibu Mkuu amewataka waendelee kuwa na imani na Mgombea wa Urais na Mwenyekiti wa CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan — kiongozi anayeendelea kuandika ukurasa mpya wa maendeleo kwa kuunganisha juhudi za wananchi na dira ya Kazi na Utu.
Dkt. Migiro amewakaribisha wananchi wa Bukombe kumpokea Dkt. Samia kwa heshima na mapenzi makubwa, akisisitiza kuwa kura ya Oktoba 29 ni kura ya maendeleo, umoja na mwendelezo wa mafanikio.