NA JOHN BUKUKU -BUKOMBE GEITA
Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema Serikali imeendelea kuwekeza katika sekta ya michezo kwa kujenga uwanja mkubwa wa kisasa katika Wilaya ya Bukombe, Mkoa wa Geita, ili kutoa fursa kwa vijana kuendeleza vipaji vyao na kukuza ajira kupitia michezo.
Akizungumza Oktoba 12, 2025, katika muendelezo wa kampeni za Chama hicho, Dkt. Samia alisema uwanja huo utakuwa kitovu cha michezo na burudani katika Kanda ya Ziwa, na kwamba Serikali itaendelea kuboresha miundombinu ya michezo nchini kote ili vijana watumie vipaji vyao kama njia ya kujipatia kipato.
Dkt. Samia aliongeza kuwa Serikali imekuwa ikiweka mkazo katika kuboresha maisha ya wananchi wa Bukombe kupitia sekta mbalimbali, ikiwemo kilimo, elimu, afya na michezo, kwa lengo la kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja na wa Taifa kwa ujumla.
Amesema, “Serikali imejenga uwanja huu wa kisasa kwa ajili ya michezo na burudani, ili vijana waweze kutumia vipaji vyao na kupata fursa za maendeleo. Tufanye kazi, tulinde na tuimarisha utu wa Mtanzania na utu wa Wanabukombe.”
Awali, Mgombea Ubunge wa Jimbo la Bukombe, Dkt. Dotto Biteko, alisema uwanja huo wa kisasa ni moja ya alama muhimu za maendeleo zilizoletwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Dkt. Samia, ambapo sasa mechi zinaweza kuchezwa mchana na usiku kutokana na uwepo wa miundombinu ya taa za kisasa.
Dkt. Biteko alisema, “Dkt. Samia amewapendelea Wanabukombe kwa kuijengea wilaya yao uwanja wa kisasa unaokidhi viwango vya kitaifa. Hii ni hatua kubwa ya maendeleo na uthibitisho wa upendo wake kwa wananchi wa Bukombe.”
Ameongeza kuwa Dkt. Samia amebadilisha sura ya Bukombe kupitia miradi mikubwa ya maendeleo, na kwamba Wanabukombe watamchagua kwa kishindo katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu kwa sababu amewapenda, kuwaamini na kuwainua kimaendeleo.