NA JOHN BUKUKU
Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameendelea leo na kampeni zake katika Mkoa wa Geita, ambako anatarajiwa kufanya mikutano mikubwa ya hadhara katika maeneo ya Masumbwe, Runzewe na Bukombe.
Ziara hiyo ni mwendelezo wa kampeni zake Kanda ya Ziwa, ambapo maelfu ya wananchi wamejitokeza kumsikiliza na kumuunga mkono kutokana na utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo chini ya serikali ya awamu ya sita.
Katika hotuba yake, Dkt. Samia aliwahimiza Watanzania kuendelea kudumisha amani, umoja na ushirikiano, akibainisha kuwa hayo ndiyo misingi mikuu ya mafanikio ya taifa.
“Maendeleo ya kweli yanatokana na ushirikiano wa wanawake na wanaume, kwani wote wamepewa uwezo sawa wa kufikiri, kupanga na kutenda. Tukishirikiana, tutajenga taifa imara lenye misingi ya heshima na amani,” alisema Dkt. Samia.
Aidha, aliahidi kuendeleza miradi mikubwa ya maendeleo katika sekta za kilimo, afya, elimu, mifugo, miundombinu na madini, akisema serikali ya CCM imeweka msingi thabiti wa kuinua uchumi wa wananchi, hususan katika maeneo ya vijijini.
Kuhusu maandalizi ya uchaguzi mkuu, Dkt. Samia aliwataka wananchi kujitoa kwa wingi kupiga kura Oktoba 29, akisisitiza kuwa zoezi hilo lifanyike kwa amani na utulivu bila vurugu wala msongamano usio wa lazima.
“Nawaomba Watanzania mjitokeze kwa wingi kupiga kura Oktoba 29. Baada ya kupiga kura, rudi nyumbani mkapumzike kwa amani mkisubiri matokeo, kwa kuwa nchi yetu ipo salama na jeshi letu lipo imara. Hakuna sababu ya hofu wala fujo,” alisisitiza Dkt. Samia.
Kwa upande wake, viongozi wa CCM mkoani Geita wamesema maandalizi yote ya mikutano hiyo yamekamilika, huku wakitoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kumsikiliza mgombea wao na kuendeleza kampeni kwa amani, upendo na umoja.