Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Cosato Chumi, ameshiriki maadhimisho ya Siku ya Taifa la Uhispania yaliyofanyika Oktoba 10, 2025, katika makazi ya Balozi jijini Dar es Salaam.
Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Chumi aliwasilisha salamu za pongezi kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa Serikali na wananchi wa Ufalme wa Uhispania.
Alisisitiza kuwa Tanzania inathamini urafiki wa muda mrefu na ushirikiano uliopo kati ya nchi hizo mbili kwa manufaa ya wananchi.
Mhe. Chumi alieleza kuwa maadhimisho hayo yanatoa fursa ya kusherehekea siyo tu historia na tamaduni za Uhispania, bali pia uhusiano wa kirafiki uliojengwa kwa muda mrefu kati ya Tanzania na Uhispania na kuahidi kuwa Serikali ya Tanzania itaendelea kuimarisha ushirikiano huo kwa manufaa ya wananchi wa pande zote mbili.
Mhe. Chumi alibainisha kuwa uhusiano wa Tanzania na Uhispania una historia ya zaidi ya miaka 58, na kwamba Uhispania imekuwa mshirika muhimu wa maendeleo katika sekta za afya, maji, umeme vijijini, na kilimo biashara na kwamba uhusiano huo ni nguzo muhimu katika kukuza maendeleo endelevu.
Akizungumza kuhusu miradi ya ushirikiano, Mhe. Chumi alitolea mfano mradi wa kurekebisha Mto Msimbazi jijini Dar es Salaam unaotekelezwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania, Benki ya Dunia, na Serikali ya Uhispania kuwa ni mradi unaonyesha dhamira ya pamoja katika kuboresha mazingira na maisha ya wananchi wa Tanzania.
Mhe. Chumi pia alitaja mafanikio ya Jukwaa la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Uhispania lililofanyika Julai 2025 huko Seville, Uhispania, na kuhudhuriwa na Makamu wa Rais wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango kuwa umefungua ukurasa mpya wa ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi hizo.
Alieleza kuwa kampuni nyingi za Kihispania zimeonyesha nia ya kuwekeza nchini katika sekta za kilimo, madini, nishati, TEHAMA, na miundombinu, jambo linaloashiria kuimarika kwa uhusiano wa kiuchumi na uwekezaji.
Aidha, Mhe. Chumi alitambua mchango wa Uhispania katika sekta ya utalii duniani na kubainisha kuwa Tanzania inapanua ushirikiano katika eneo hilo na kumualika Balozi Paloma Robles kutumia blogu na picha zake kutangaza vivutio vya utalii vya Tanzania, na kwamba anaweza kuwa balozi mzuri wa utalii wa Tanzania.
Naye, Balozi wa Ufalme wa Uhispania nchini, Mheshimiwa Paloma Robles, alisisitiza dhamira ya Serikali ya Uhispania kuendeleza uhusiano wa kidiplomasia, kiuchumi, na kijamii na Tanzania na kwamba Uhispania inatambua mchango wa Tanzania katika kudumisha amani na maendeleo barani Afrika.
Balozi Robles alisema maadhimisho ya Siku ya Taifa la Uhispania ni ishara ya urafiki, ushirikiano, na maelewano ya kweli kati ya wananchi wa Tanzania na Uhispania, akiahidi kuendelea kushirikiana katika nyanja zote kwa manufaa ya wananchi wa pande zote mbili.
Maadhimisho ya Siku ya Taifaya Uhispania nchini yailihudhuriwa na mabalozi wa nchi mbalimbali, viongozi wa serikali na wageni waalikwa.