NA JOHN BUKUKU- SIMIYU
Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, anaendelea leo na kampeni zake katika mikoa ya Simiyu na Shinyanga, ambapo anatarajiwa kufanya mikutano mikubwa ya hadhara katika maeneo ya Maswa, Shinyanga Mjini na Kahama Mjini.
Ziara hiyo ni mwendelezo wa kampeni zake Kanda ya Ziwa, baada ya jana kufanya mikutano mikubwa katika wilaya za Serengeti na Bariadi, ambako alisisitiza masuala muhimu kuhusu umoja wa kitaifa, usalama wa uchaguzi na maendeleo ya wananchi.
Katika mkutano uliofanyika Serengeti, Dkt. Samia alihimiza ushirikiano kati ya wanaume na wanawake bila ubaguzi, akisema kuwa maendeleo ya taifa yanapatikana pale ambapo Watanzania wote wanashirikiana bila kujali jinsia, kabila au mila.
“Maendeleo ya kweli yanatokana na ushirikiano wa wanawake na wanaume, kwani wote wamepewa uwezo sawa wa kufikiri, kupanga na kutenda. Tukishirikiana, tutajenga taifa imara na lenye misingi ya heshima na amani,” alisema Dkt. Samia.
Pia aliahidi ujenzi wa uwanja wa kisasa wa Serengeti, utakaosaidia kukuza utalii wa ndani na kuongeza fursa za ajira kwa vijana wa eneo hilo.
Katika mkutano wa Bariadi mkoani Simiyu, Dkt. Samia aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura siku ya uchaguzi mkuu Oktoba 29, akiwahakikishia kuwa serikali imejipanga kikamilifu kuhakikisha nchi inabaki salama, yenye amani na utulivu.
“Nchi yetu ipo salama, jeshi letu lipo imara, hivyo wananchi msihofu. Jitokezeni kwa wingi kupiga kura kwa amani na utulivu, ili tuchague viongozi wa kuendelea kuijenga Tanzania yetu,” alisisitiza.
Katika hotuba yake, aligusia pia utekelezaji wa miradi mikubwa katika sekta za kilimo, afya, elimu, mifugo na miundombinu, akisema serikali ya CCM imewekeza kwa kiwango kikubwa katika huduma hizo ili kuboresha maisha ya Watanzania wote.
Leo, Dkt. Samia anatarajiwa kuendelea na kampeni hizo katika maeneo ya Maswa, Shinyanga Mjini na Kahama Mjini, ambapo atazungumza na wananchi kuhusu vipaumbele vya serikali katika miaka ijayo na kusisitiza umuhimu wa kudumisha amani wakati wote wa kipindi cha kampeni na uchaguzi.