Mfanyabiashara wa vipodozi anayefanya shughuli zake katika eneo la stendi ya zamani Mfaranyaki Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma Matilda Kapinga kushoto,akiwasilikiza mafundi wa Shirika la Umeme Tanzania(Tanesco)kabla ya kufungiwa mita mpya za umeme(mita janja) kwa ajili ya kuboresha huduma za upatikanaji wa nishati ya umeme.
Mafundi wa Shirika la umeme Tanzania(TANESCO)Mkoa wa Ruvuma wakijiandaa kuwafungia wateja mita mpya katika eneo la stendi ya zamani ya Mfaranyaki Songea mjini.
………..
Na Mwandishi Maalum, Ruvuma
Shirika la Umeme Tanzania(TANESCO) Mkoani Ruvuma,limeanza kuwafungia wateja mita mpya(Mita Janja) ambazo mteja ataweza kulipia na kuingiza kwenye mita moja kwa moja kama inavyofanyika kwenye ving’amuzi.
Hayo yamesemwa na Mhandisi wa Shirika hilo Malibe Boniphace,wakati wa zoezi la kuondoa mita za zamani na kufunga mpya kwa wateja wake katika eneo la Stendi ya zamani Mfaranyakati Manispaa ya Songea Wilayani Songea.
“Kazi ya kufunga mita janja ambazo zinamwezesha mteja kununua na kuingiza umeme moja kwa moja ilianza tangu mwaka jana katika mikoa mbalimbali,lakini hapa Ruvuma tumeanza kutekeleza mpango huu unaokwenda sambamba na maadhimisho ya wiki ya huduma kwa wateja”alisema Malibe.
Alisema,wanapita katika maeneo mbalimbali kuwafungia wateja mita janja ili kuboresha huduma hasa ikizingatia kuwa mita hizo zina faida nyingi ikiwemo kuwaondolea wateja usumbufu wa Kwenda kwenye mita kwa ajili ya kuingiza umeme.
“Mita hizi ni bora sana kwani mteja ukiwa kitandani unaweza kuingiza umeme moja kwa moja,kwa hiyo tumeanza zoezi ili na kupitia wiki ya huduma tunakwenda kwa wateja wetu kuwafungia mita mpya”alisema Malibe.
Alisema,Tanesco Mkoa wa Ruvuma kupitia wiki ya huduma kwa wateja imejipanga kuboresha huduma kwa kubadilisha nguzo za zamani na kuweka nyingine za zege ili kuondoa changamoto ya ukatikaji wa umeme mara kwa mara hasa kipindi cha mvua.
Malibe ametaja mikakati mingine ni kutoa huduma za kuunganisha umeme kwa muda mfupi mara mteja anapoomba na kulipia anafanyiwa ukaguzi na kupata huduma haraka,kuimarisha mindombinu na kushughulikia matatizo na kuyatatua na kumuunganishia mteja umeme.
“Mkoa wa Ruvuma,tumejipanga kuhakikisha kuwa kati ya malengo yetu tuliyojiwekea ni kubadilisha mitazamo hasi iliyojengeka kwa wateja wetu,kwa kuhakikisha huduma kwa wateja wetu zinakuwa bora na kwa wakati”alisema.
Baadhi ya wateja waliofungiwa mita hizo,wameipongeza Tanesco kwenda sambamba na karne ya Sayansi na teknolojia ambayo sehemu kubwa ya watu wake wameachana na vitu vya zamani ambavyo uwendesha wake unatumia nguvu na gharama kubwa.
Matilda Kapinga mfanyabiashara wa eneo la stendi ya zamani Manispaa ya Songea,ameishukuru Tanesco kufika mtaani kwao kuwafungia mita za Kidijital ambazo zitawaondolea usumbufu mkubwa wa kupanda juu ya nguzo ili kuingiza umeme kwenye mita.
Alisema, hiyo ni hatua kubwa kwa shirika hilo ambapo ameyataka mashirika na taasisi nyingine za umma zilizopo Mkoa wa Ruvuma, kubadilika kiutendaji na kufanya kazi kwa weledi.
Saad Abdul mfanyabiashara wa Duka la kubadilisha fedha alisema,Tanesco imeonyesha kukua na kubadilika kiutendaji kwani wanapata huduma haraka tofauti na miaka ya nyuma ambapo ili kuunganishiwa umeme mteja alilazimika kusuiri kati ya miezi miwili hadi mitatu.
Alisema,kila mmoja anahitaji huduma bora,hivyo mtu akienda Tanesco na akipata huduma haraka na kuondoka na kwenda kwenye shughuli zake hawezi kulalamika badala yake atakuwa balozi mzuri.