Na Mwandishi wetu, Mirerani
MKUU wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, mwalimu Fakii Raphael Lulandala amezindua kampeni ya kutoa elimu kwa jamii kushiriki uchaguzi mkuu kwa kujitokeza kwa wingi kupiga kura Oktoba 29 mwaka huu wa 2025 kupitia tamasha la Simanjiro Vote & Vibe Festival.
Mwalimu Lulandala akizungumza kwenye tamasha hilo lililofanyika mji mdogo wa Mirerani, amesema lengo ni jamii kufurahia buridani na kupata ujumbe wa kushiriki uchaguzi kupitia kauli mbiu ya kura yako sauti yako.
Amewahakikishia wakazi wa wilaya hiyo kuwa uchaguzi mkuu wa mwaka huu wa 2025 utafanyika kwa amani hivyo wajitokeze kwa wingi wakawachague viongozi wanaowapenda.
“Msisikilize kelele za baadhi ya watu wanaodhani kuwa uchaguzi hautafanyika, msiwasikile hao ninyi jiandaeni tuu siku ya uchaguzi mjitokese kwa wingi mkapige kura bila wasiwasi wowote ule,” amesema DC Lulandala.
Afisa michezo wa Simanjiro Juliana Kiwara amesema michezo mbalimbali ikiwemo soka, pete, wavu, kukimbiza kuku, kuvuta kamba, kunywa soda na mkate, imefanyika katika tamasha hilo.
Kiwara amesema tamasha hilo limeshirikisha timu kutoka Wilaya za Simanjiro na majirani zao kutoka Wilaya ya Hai Mkoani Kilimanjaro na Halmashauri ya Wilaya ya Meru Mkoani Arusha.
Mratibu wa tamasha hilo Charles Mnyalu amempongeza mkuu huyo wa wilaya kwa kuandaa tamasha hilo ambapo jamii imepata burudani na kusikia ujumbe wa kushiriki uchaguzi kwa kupiga kura.
“Tamasha lilikuwa zuri na lenye kuwafurahisha watu walioshiriki na wamesimia ujumbe kuwa wanatakiwa kutumia haki yao ya msingi kwa kupiga kura,” amesema Mnyalu.
Mkazi wa mji mdogo wa Mirerani, Ester Sumary amesema tamasha la Simanjiro Vote & Vibe Festival limewapa hamasa ya kushiriki kupiga kura.
“Pia tumejionea burudani mbalimbali za muziki, michezo tofauti ya mpira, hakika jamii imefurahi na tutatimiza malengo yetu kwa kuwachagua viongozi tunaowapenda kwa mgombea urais, ubunge na udiwani,” amesema Sumary