JUKWAA la Wahariri Tanzania (TEF) limeeleza kusikitishwa na taarifa zinazosambaa mitandaoni kuanzia Oktoba 6, 2025, kuhusu tukio la utekaji lililoripotiwa kutokea jijini Dar es Salaam, na kuitaka jamii kulaani matendo hayo yasiyo ya kibinadamu.
TEF imesema tukio hilo linawakumbusha Watanzania matukio yaliyowahi kutokea huko nyuma ya utekaji wa watu mbalimbali, pamoja na mauaji ya kikatili yaliyoshuhudiwa katika vipindi tofauti, ambayo yamekuwa yakipoteza taswira ya amani ambayo taifa limejijengea kwa muda mrefu.
Kwa mujibu wa taarifa za awali, Jeshi la Polisi limethibitisha kupokea taarifa za tukio hilo na linaendelea na uchunguzi ili kubaini ukweli wake.
Katika tamko lake, TEF imesisitiza kuwa uhai na usalama wa kila Mtanzania ni kipaumbele cha kwanza katika kudumisha amani ya taifa, ikibainisha kuwa amani ni matokeo ya haki. Jukwaa hilo limeuliza maswali mazito kuhusu chanzo cha matukio hayo, likitaka mamlaka husika kubaini kwa haraka wanaohusika na sababu za vitendo hivyo kuendelea kujitokeza.
TEF imelitaka Jeshi la Polisi kuchunguza kwa umakini na kwa kasi ili kubaini ukweli wa tukio hilo, kisha kulijulisha taifa kwa uwazi nini kimetokea na kuhakikisha wahusika wanachukuliwa hatua stahiki za kisheria.
Aidha, Jukwaa hilo limekemea vikali matendo ya utekaji na kutoa wito kwa wanasiasa, wafuasi wa vyama na Watanzania wote kushiriki katika siasa za hoja badala ya chuki, visasi au vitendo vinavyohatarisha usalama wa watu.