Na Mwandishi wetu, Ngorongoro
Tarehe 7 Oktoba, 2025.
Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro imewashirikisha baadhi ya watalii katika uzinduzi wa wiki ya huduma kwa wateja ambapo wageni hao wameipongeza mamlaka hiyo kwa kuendelea kuboresha huduma na miundo mbinu ya utalii.
Wakizungumza katika hafla iliyofanyika kwenye lango kuu la kuingia Hifadhi ya Ngorongoro eneo la Loduare baadhi ya watalii hao wamesema kuwa wanaridhishwa na huduma zinazotolewa na mamlaka hiyo na kusema wataendelea kuwashawishi wageni wengine kutoka nchi zao kutembelea Ngorongoro.
Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa uhifadhi anayeshughulikia Huduma za Utalii Mariam Kobelo amewahakikishia wageni hao kuwa mamlaka itaendelea kuboresha huduma zake na kwamba watafanyia kazi kwa ukaribu maoni yote yatakayotolewa na wateja ili kuendelea kuunga mkono juhudi za serikali za kuongeza wageni katika sekta ya utalii.
“Tunaitumia wiki hii ya huduma kwa wateja kuendelea kupokea maoni mbalimbali ya wateja wetu,tumejipanga vizuri kuhakikisha kuwa tunashughulikia maoni yote yatakayotolewa ili kuunga mkono kwa vitendo juhudi za serikali yetu za kuboresha utalii nchini,”alisema Mariam.
Wiki ya Huduma kwa wateja ni mahsusi kwa ajili ya kutoa nafasi kwa watumishi wa sekta mbalimbali kuwasikiliza wateja wao na kufanyia kazi maoni ya wateja wao.