Mgombea wa nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa Ndugu Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza na wananchi wa Kata ya Buhongwa, katika muendelezo wa Kampeni za Uchaguzi kwa CCM, Nyamagana mkoani Mwanza tarehe 07 Oktoba 29, 2025.
……………..
NA JOHN BUKUKU- MWANZA
Mgombea wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameahidi kuongeza bajeti ya ujenzi wa barabara zinazohudumiwa na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) ili kuboresha mtandao wa barabara Jijini Mwanza na kuhakikisha zinajengwa kwa viwango vinavyokubalika.
Akizungumza leo, Jumanne Oktoba 7, 2025, katika eneo la Buhongwa, Wilaya ya Nyamagana, akiwa kwenye siku yake ya kwanza ya kampeni mkoani humo, Dkt. Samia amesema hatua hiyo inalenga kuimarisha upatikanaji wa huduma za usafiri na kukuza maendeleo ya kiuchumi katika jiji hilo.
Amefafanua kuwa Serikali itatekeleza ujenzi wa barabara ya Mwanza City Centre–Buhongwa–Usagara, ambayo itakuwa na njia nne, na kueleza kuwa mchakato wa kumpata mkandarasi uko katika hatua za mwisho baada ya tenda kutangazwa.
Aidha, ameeleza kuwa Serikali pia imepanga kutekeleza ujenzi wa barabara za Mwanza City Centre–Igoma–Kisesa pamoja na Mkuyuni–Maina–Muhangu–Igoma, ambazo tayari zimefanyiwa upembuzi yakinifu na maandalizi ya ujenzi yanaendelea.
Akizungumzia utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2020–2025, Dkt. Samia amesema Serikali imekamilisha ujenzi wa barabara ya Buhongwa–Igoma yenye urefu wa kilomita 14 kwa gharama ya shilingi bilioni 22.7, sambamba na madaraja ya Mkuyuni na Mabatini ambayo yamegharimu shilingi bilioni 11.2. Amesisitiza kuwa atahakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.
Shamra shamra za mapokezi ya Mgombea wa nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa Ndugu Dkt. Samia Suluhu Hassan mara baada ya kuwasili Buhongwa mkoani Mwanza tarehe 07 Oktoba, 2025.
Sehemu ya Wananchi wa Kata ya Buhongwa waliohudhuria mkutano wa hadhara wa Kampeni wa Mgombea wa nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa Ndugu Dkt. Samia Suluhu Hassan mkoani Mwanza tarehe 07 Oktoba, 2025.