*Aahidi kujenga barabara za juu, kuboresha soko la Kariakoo kuwa la kisasa lenye barabara za chini, na kuunda mfumo wa biashara wa saa 24 jijini Dar es Salaam.
DAR ES SALAAM
Mgombea urais kupitia Chama cha NLD, Mhe. Doyo Hassan Doyo, ameendelea na kampeni zake kwa kasi jijini Dar es Salaam kupitia mtindo wa kipekee wa “Mobile Kampeni”, mfumo unaomuwezesha kufanya mikutano mingi kwa siku moja katika maeneo mbalimbali.
Leo, Mhe. Doyo amefanya mikutano ya kampeni katika maeneo tofauti ya jiji la Dar es Salaam, ikiwemo Temeke, Ilala, na Mbande Center.
Aidha, amefika katika majimbo ya Chamazi, Mbagala, Temeke, Kivule, Ukonga, na Segerea, ambapo amewahutubia wananchi katika maeneo kama Soko la Kizuiani, Tandika Sokoni, Kitunda Lerini, Mazizini, na kumalizia kampeni katika eneo la Mnyamani Lerini.
Katika mikutano hiyo, Mhe. Doyo ameendelea kusisitiza dhamira ya chama chake ya kuleta mabadiliko chanya ya kiuchumi, kijamii, na kiutawala, huku akiwataka wananchi wa Dar es Salaam kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura.
Amesema kuwa “Tanzania ni kisiwa cha amani na utulivu, na jukumu letu ni kuilinda kwa kufanya maamuzi sahihi wakati wa uchaguzi.”
Akiwahutubia baadhi ya wakazi wa jiji la Dar es Salaam, Mhe. Doyo alisema kuwa Dar es Salaam ndio sura na kitovu cha biashara Tanzania, na kwamba serikali yake itatekeleza sera madhubuti za kulibadilisha jiji hilo kuwa kituo cha kisasa cha biashara na uchumi cha Afrika Mashariki.
Miongoni mwa mipango yake ni kujenga barabara za juu 54 zenye umbali mrefu, hatua itakayosaidia kuondoa msongamano mkubwa wa magari na kuhakikisha wananchi wanatembea na kufanya shughuli zao kwa ufanisi bila kupoteza muda barabarani.
Aidha, atatekeleza mfumo wa barabara za chini ili kurahisisha usafiri wa kila siku. “Tutaibadilisha Dar es Salaam kuwa jiji lenye mtiririko wa usafiri wa uhakika, usio na msongamano, ili kila mwananchi anufaike na uchumi kwa muda mfupi,” alisema Doyo.
Kuhusu soko la Kariakoo, Mhe. Doyo alisema serikali yake itatekeleza mpango wa kuliboresha na kuligeuza kuwa soko la kisasa lenye miundombinu ya chini kwa chini, ikiwemo maduka ya kisasa, maghala, na barabara ndogo za kupita magari madogo chini ya ardhi, hatua itakayosaidia kuondoa foleni na msongamano mkubwa juu. “Tutaunda mfumo wa biashara wa saa 24 kwa siku. Hii itafungua ajira, kuongeza mapato ya serikali, na kuimarisha uchumi wa jiji letu la kibiashara, huku tukizingatia usalama wa wafanyabiashara,” aliongeza
Aidha, Mhe. Doyo amesisitiza kuwa serikali yake itafuta mfumo wa ajira portal, mfumo ambao kwa sasa hautendi haki kwa vijana wengi wa Kitanzania.
Amesema mfumo huu unazuia vijana wenye sifa kupata ajira kwa sababu nafasi zinatolewa kwa vimemo au kwa upendeleo wa kisiasa. “Serikali yangu itahakikisha mfumo huu unaondolewa, ili kila kijana wa Kitanzania mwenye sifa na uwezo apate nafasi ya ajira. Hii ni ahadi yangu kwa vijana wote wa Dar es Salaam na taifa kwa ujumla,” alisema Mhe. Doyo.
Mhe. Doyo ameeleza kuwa ajira zitatolewa kwa sifa, usawa, na uadilifu, bila kuzingatia uhusiano wa kisiasa au upendeleo kutoka katika mfumo wa ajira portal. Wale wote waliopata ajira kwa njia zisizo halali wataondolewa, na nafasi hizo zitatolewa kwa watanzania wenye sifa halisi, ili kukuza mfumo wa ajira unaozingatia usawa katika taifa.
Mhe. Doyo ameahidi kusimamia sera ya mikopo yenye riba nafuu au isiyo na riba kabisa, ili wafanyabiashara wadogo na vijana wajikwamue kiuchumi. Amesisitiza kuwa mikopo isiyo na riba, ni mbinu pia ya uhamasishaji wa ulipaji kodi kwa hiari, ambapo Watanzania wataona manufaa ya kodi zao na kujitolea kulipa badala ya kulazimishwa. “Tutajenga mfumo wa kodi unaompa heshima mlipakodi. Mtanzania atalipa kwa hiari kwa sababu ataona manufaa yake, huku kichoche cha ulipaji kodi kwa hiari ikiwa ni mikopo isiyo na riba,” alisema Domo.
Mhe. Doyo amewataka wananchi wa Dar es Salaam na Watanzania kwa ujumla kuchagua viongozi kutoka NLD, viongozi waadilifu na wachapakazi, ambao wanajali maslahi ya wananchi na mustakabali wa taifa.
Amesema kampeni zake ni za amani, umoja na matumaini mapya kwa Watanzania wote. “Tunakwenda kuijenga Tanzania mpya kupitia NLD, Tanzania yenye usawa, uchumi imara, na fursa sawa kwa kila mwananchi, tukiwa tunaongozwa na tunu ya uzalendo, haki, na maendeleo,” alihitimisha Doyo.
Msafara wa mgombea urais huyo kesho utakuwa katika wilaya ya Kinondoni kabla ya kuelekea Morogoro, ambapo Mhe. Doyo ataendelea na mikutano ya kampeni na kuwasilisha sera zake kwa wananchi.