NA DENIS MLOWE, IRINGA
FADHILI Ngajilo mgombea ubunge Iringa mjini kwa tiketi ya CCM amesema kwamba endapo akichaguliwa atalivalia njuga suala la wafanyabiashara ya Kitanzini – Miyomboni kufanya biashara masaa 24 kutokana kata hiyo kuwa ya wafanyabiashara wengi.
Ngajilo alisema kwamba jimbo la Iringa mjini linaongozwa na wafanyabiashara ambao asilimia kubwa wako katika kata ya Kitanzini Miyomboni ambapo kuna soko kuu la Iringa, soko la Magari mabovu na kila aina ya biashara halalli inafanyika hapo hivyo kuna umuhimu wa kuanzisha biashara masaa 24.
Alisema ili kufanikisha hilo watakaa chini kama halmashauri na kuketi na jeshipolisi kulinda usalama wa wafanyabiashara na kufungwa mataa kwa ajili ya usalama kwa maeneo ya kata hizo.
Alisema kuwa nchi nyingi duniani wanafanya biashara usiku na aliyesema watu walale usiku ni nani alihoji Ngajilo na kuongeza kuwa lengo ni kuinua kipato cha mwananchi wa jimbo la Iringa.
Alisema endapo atapewa ridhaa hiyo na wananchi wataichagua serikali iongozwe na CCM watahakikisha wanajjenga Machinga Complex ambalo wafanyabiashara watafanyia biashara kwa utulivu.
Aidha aliongeza kuwa watahakikisha kwa kushirikiana na diwani wa Miyomboni Kitanzini watarekebisha soko la Kitanzani liwe la kisasa kuliko lilivyo sasa.
Ngajilo akizungumzia kuhusu Suala la makazi katika kata hiyo atahakikisha yanarasimishwa kwa wale ambao bado na kuhakikisha wanapata vibali vya kukarabati makazi kwa wakati.
Suala la afya alisema kuwa wataendelea kuongeza idadi ya vituo vya afya ambavyo viko katika ilani ya CCM na kuwataka wananchi wawape kura za kishindo katika mafiga matatu kwa maana ya Rais Samia , wabunge na madiwani.
Vilevile alisema kuwa Ngajilo Cup itaendelea ndani ya jimbo la Iringa ambapo kuhusu michezo mingine kama ndondi , atahakikisha inakua na kuwa chanzo cha ajira kwa vijana.