NA JOHN BUKUKU – DODOMA
DODOMA, Oktoba 5, 2025
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesisitiza umuhimu wa Watanzania wote kulinda amani, umoja na utulivu wa nchi kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025, kikibainisha kuwa amani ndiyo nguzo ya maendeleo na mafanikio ya taifa.
Akizungumza na vyombo vya habari leo katika Makao Makuu ya CCM, Dodoma, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Bw. Kenani Kihongosi, amesema kampeni za CCM zimekuwa zikifanyika kwa amani na kuungwa mkono na wananchi wengi kote nchini, jambo linalodhihirisha ukomavu wa kisiasa wa Watanzania na jinsi wanavyothamini tunu ya amani.
“Tangu kuzinduliwa kwa kampeni za urais tarehe 28 Agosti 2025 katika Viwanja vya Tanganyika Packers, Kawe, Dar es Salaam, mgombea wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya mikutano 77 katika mikoa 21, ikihudhuriwa na zaidi ya watu milioni 14.6, huku zaidi ya milioni 31 wakifuatilia kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii. Mikutano yote imefanyika kwa utulivu mkubwa,” alisema Kihongosi.
Amesema mafanikio yaliyopatikana chini ya uongozi wa Dkt. Samia katika kipindi cha miaka minne ndiyo yameendelea kuongeza imani ya wananchi kwa CCM, yakiwemo maendeleo katika miundombinu, afya, elimu, maji, uchumi na ajira.
“Dkt. Samia amesimamia miradi mikubwa ya kimkakati kama Bwawa la Julius Nyerere lililofikia asilimia 99.55, Reli ya Kisasa (SGR) kutoka Dar es Salaam hadi Makutupora, pamoja na ujenzi wa barabara zenye jumla ya kilomita 15,366.36. Haya yote yamefanyika katika mazingira ya amani na utulivu,” aliongeza Kihongosi.
Akitaja mafanikio mengine, alisema ndani ya miaka minne vituo 1,368 vya afya vipya vimejengwa, hospitali za dharura zimeongezeka kutoka saba hadi 116, shule za msingi zimeongezeka hadi kufikia 19,783, na bajeti ya mikopo ya elimu ya juu imeongezeka kutoka Shilingi bilioni 464 hadi 786.
Bw. Kihongosi alibainisha kuwa mafanikio hayo yamechagizwa na falsafa ya utu, usawa na maendeleo kwa wote ambayo yamekuwa dira ya Dkt. Samia, ikiwemo kuwajali wafanyakazi, kuanzisha huduma za matibabu bure kwa wagonjwa wa saratani, figo na kisukari, pamoja na kutoa bima ya afya kwa wazee na walemavu.
Kadri siku za kuelekea uchaguzi zinavyopungua, Kihongosi amesema CCM imejipanga kuhakikisha kampeni zinaendelea kwa amani huku wananchi wakihamasishwa kujitokeza kwa wingi kupiga kura kwa utulivu.
“Tunapokaribia uchaguzi huu muhimu, wito wa mgombea wetu wa urais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuendelea kufanya kampeni za kistaarabu, zinazozingatia utu wa Mtanzania. Wito zaidi ni kwa kila Mtanzania kuwa mlinzi wa amani ya nchi, kwani amani na utulivu ndiyo tunu yetu ya Taifa,” alisisitiza.
Ameongeza kuwa Dkt. Samia anatarajiwa kuanza rasmi ziara yake ya kampeni Kanda ya Ziwa kuanzia Oktoba 7, 2025, ambapo ataendelea kuhimiza umoja na mshikamano wa kitaifa kama nguzo ya maendeleo endelevu ya Tanzania.
“CCM tumejipanga kikamilifu kuhakikisha tunamfikia kila Mtanzania na kumhamasisha akapige kura kwa amani na utulivu. Ushindi wa kishindo ni muhimu, lakini zaidi ya yote, tunalinda amani ya nchi yetu,” alisema Kihongosi.