Na Fullshangwe Media, Sikonge
Sikonge, Tabora — Mgombea mwenza wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Emmanuel John Nchimbi, leo Oktoba 5, 2025, ameendelea na mikutano yake ya kampeni kwa kufanya mkutano wa hadhara uliofanyika eneo la TASAF, katika Jimbo la Sikonge, mkoani Tabora.
Katika mkutano huo uliovuta mamia ya wananchi, Dkt. Nchimbi alitumia nafasi hiyo kuwanadi wagombea wa CCM katika nafasi mbalimbali, akiwemo Mgombea Ubunge wa Jimbo la Sikonge, Mhandisi Amosy William Maganga, pamoja na wagombea wa Udiwani katika kata mbalimbali za jimbo hilo.
Akizungumza na wananchi, Dkt. Nchimbi aliwahimiza kujitokeza kwa wingi katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, ili kumpa ushindi mkubwa Mgombea Urais wa CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan, akisisitiza kuwa rekodi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo chini ya uongozi wake ni ushahidi tosha wa uadilifu na uchapakazi.
“Dkt. Samia ameonyesha dira ya kweli ya maendeleo kwa Watanzania wote. Amewekeza katika miundombinu, elimu, afya na uwezeshaji wa vijana na wanawake. Kumpa kura ni kuendeleza kasi hii ya maendeleo,” alisema Dkt. Nchimbi huku akishangiliwa na wananchi.
Mkutano huo ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa CCM mkoani Tabora, ambao walitoa wito kwa wananchi kuendelea kudumisha amani na mshikamano wakati wa kipindi cha kampeni na kuelekea siku ya uchaguzi.
Dkt. Nchimbi anaendelea na ziara yake ya kampeni mkoani Tabora, ikiwa ni mkoa wa 18 kati ya mikoa anayoizunguka nchini, kwa lengo la kumuombea kura Mgombea Urais wa CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na wagombea wa Ubunge na Udiwani.