Pantaleo Mushi, mkazi wa Mbezi Beach.
………….
Wananchi wa Mkoa wa Dar Es Salaam wamesema wapo tayari kushiriki kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, wakisisitiza umuhimu wa kudumisha amani na utulivu nchini. Wameeleza kuwa hawatishwi na kampeni zinazoenezwa mitandaoni zinazohamasisha maandamano na kutojitokeza kupiga kura, wakisema wanaelewa vyema athari za vurugu zikiwemo vifo, majeraha na kuporomoka kwa uchumi kunakotokana na kukosekana kwa utulivu wa kijamii na kiuchumi.
Pantaleo Mushi, mkazi wa Mbezi Beach, amesema anafahamu jukumu lake la kikatiba la kupiga kura na amewahamasisha vijana wengine kujitokeza kwa wingi kutumia haki yao hiyo, ili kuchagua viongozi wanaowataka. Amesema kutopiga kura ni sawa na kumpa nafasi kiongozi usiyemtaka kushika madaraka kwa kipindi cha miaka mitano ijayo katika ngazi ya kata, jimbo na hata urais.
Kwa upande wao, Said Nassor na Yusuph Ibengwe, wakazi wa Kawe, wameeleza kutofahamu lolote kuhusu maandamano na kusisitiza kuwa wananchi hawapaswi kurubuniwa kuharibu amani ya Tanzania kwa maslahi binafsi ya baadhi ya wanasiasa. Wamewahimiza Watanzania wote kujitokeza kwa wingi siku ya Oktoba 29, 2025 kupiga kura kwa amani, na kuepuka vurugu au kusalia vituoni bila sababu kwa kisingizio cha kulinda kura.
Kulingana na baadhi ya wachambuzi wa siasa, mabadiliko ya kweli yanaanzia kwenye sanduku la kura, na iwapo mtu hatapiga kura, mwingine ataamua hatma yake. Wamekumbusha kuwa kupiga kura si haki tu bali pia ni wajibu wa raia. Wamewahimiza wananchi kutokubali kupoteza sauti zao, kwa kuwa kura yao ina thamani kubwa katika kujenga jamii wanayoitaka sasa na kwa vizazi vijavyo.
Yusuf Anyasime Ibengwe mkazi wa mkazi wa Kawe Dar es Salaam.
Said Nassor Mkazi wa Ukwamani Dar es Salaam.